KIVUMBI KIKALI, VIKUMBO KUONEKANA BONNAH SEGEREA CUP

Mbunge wa Segerea, Bonnah Kamoli na Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, wakikabidhi jezi kwa kiongozi mmoja wa timu inayoshiriki mashindano ya Bonnah Seregea Cup.

Na Nora Damian, The Page

Mashindano ya soka kuwania Bonnah Segerea Cup yanatarajia kuanza Aprili 5 yakitajwa kuwa na kishindo na ushindani mkubwa.

Mashindano hayo yanayoshirikisha timu 64 kutoka katika mitaa na makundi mbalimbali yameandaliwa na Mbunge wa Segerea, Bonnah Kamoli.

Akizungumza leo Aprili 2,2024 wakati wa uzinduzi wa mashindano hayo Bonnah amesema yanalenga kuibua na kukuza vipaji vya vijana sambamba na kuwapatia fursa mbalimbali.

“Nimekuwa nikiandaa mashindano haya kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM hasa ikizingatiwa kwamba michezo ni ajira na afya. Kupitia michezo tutaweza pia kuimarisha ulinzi na usalama kwenye maeneo yetu,” amesema Bonnah.

Akizungumza katika hafla hiyo Bonnah amesema mashindano hayo yanalenga kuibua na kukuza vipaji vya vijana sambamba na kuwapatia fursa mbalimbali.

“Nimekuwa nikiandaa mashindano haya kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM hasa ikizingatiwa kwamba michezo ni ajira na afya. Kupitia michezo tutaweza pia kuimarisha ulinzi na usalama kwenye maeneo yetu,” amesema Bonnah.

Mshindi atajinyakulia Sh milioni 5 wakati wa pili atazawadiwa Sh milioni 3 na wa tatu Sh milioni 2.

Aidha katika mchezo wa rede utakaoratibiwa na UWT Ilala bingwa atazawadiwa Sh milioni 2, mshindi wa pili atazawadiwa Sh milioni 1 na wa tatu Sh 500,000.

Mashindano hayo yatakayoanza kutimua vumbi Aprili 5 hadi Juni 2,2024 yanashirikisha timu 61 za mitaa yote ya jimbo hilo na timu tatu za makundi ya waendesha bajaji, bodaboda na Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM).

Naye Katibu wa Wenyeviti wa Serikali za Mitaa katika jimbo hilo, Thomas Temsa, amesema mashindano hayo yameongeza hamasa kwa vijana kushiriki michezo na kukuza vipaji vyao.

“Mheshimiwa mbunge amefanya kazi kubwa, kwanza anaimarisha mahusiano kati yetu wenyeviti na kutujengea uelewa mpana. Mashindano haya yatakuwa sehemu ya hamasa kwa vijana kujitokeza kwa wingi kushiriki kujiandikisha kupiga kura, tuwashawishi na tuwashirikishe,” amesema Temsa.

Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Ilala, Said Sidde, amesema Bonnah anatekeleza Ilani ya Uchaguzi kwani ibara ya 242 na 243 zinasisitiza juu ya michezo.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, amempongeza Bonnah kwa kuandaa mashindano hayo ambayo yataleta chachu ya maendeleo na kuimarisha umoja na mshikamano kuanzia ngazi ya mtaa, kata hadi wilaya.

“Vijana watapata nafasi ya kujua afya zao zikoje, tumetoa maelekezo kwamba kutengwe muda wa dakika 20 vijana wawe wanapewa elimu kuhusu masuala ya afya na maadili. Polisi kata nao watoe elimu ya namna ya kuimarisha ulinzi na usalama kwenye maeneo yao,” amesema Mpogolo.

Amesema kupitia mashindano hayo vijana wataelimishwa juu ya umuhimu wa kujiandikisha kwa ajili ya maandalizi ya kupiga kura katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 na Uchaguzi Mkuu 2025.

Aidha amewaasa vijana kutumia mashindano hayo kuzungumzia masuala yao ya kiuchumi ili waweze kuchangamkia fursa za mikopo inayotolewa na halmashauri ambapo wametenga Sh bilioni 11 kwa mwaka 2024/25.

Mkuu huyo wa wilaya amesema pia kupitia mashindano hayo na mengine yanayoandaliwa katika majimbo ya wilaya hiyo inawezekana kuunda timu ya wilaya itakayoshiriki ligi mbalimbali hadi ligi kuu.

Katika uzinduzi huo mbunge huyo pia aligawa jezi kwa timu zote shiriki.

Powered by Blogger.