MATUMIZI YA AKILI MNEMBA YABAINISHE FAIDA, ATHARI – DK. KIJAJI

Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara, Dk. Hashil Abdallah, akizungumza wakati wa kilele cha maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kumlinda Mlaji yaliyofanyika Dar es Salaam.


Na Nora Damian, The Page

Serikali imeelekeza matumizi ya akili mnemba (artificial intelligence) katika huduma za mlaji yabainishe faida na athari ili kuwezesha kubuniwa kwa taratibu zitakazomlinda mlaji.

Akili mnemba ambayo imezoeleka kutamkwa kama 'akili bandia' ni teknolojia inayokua kwa kasi na ambayo imesambaa duniani kote.

Maelekezo hayo yametolewa leo Machi 15,2024 na Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Ashatu Kijaji, katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dk. Hashil Abdallah, wakati wa kilele cha maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kumlinda Mlaji yaliyofanyika Dar es Salaam.


Amesema dunia ndiko inakoelekea na Tanzania inabidi kuwa tayari kukabiliana na teknolojia hiyo kwa kuwa yenyewe si kisiwa.

“Walaji wana hofu kuhusu namna ambavyo mfumo huduma inayotumia akili mnemba inavyoundwa, mifumo hii kwa kiasi kikubwa inahitaji taarifa nyingi katika kufanikisha uundwaji na utendaji wake.

“Hivyo tunapaswa kuhoji na kutafiti namna ambavyo mifumo hii inaundwa na kusimamiwa na endapo haya yatafanyika kwa namna inayolinda masilahi ya mlajI ni dhahiri itatusaidia kufikia malengo,” amesema Dk. Kijaji.

Aidha ametoa wito kwa wadau husika kujipanga vyema kama taifa ili kunufaika na fursa zinazotokana na akili mnemba kwa kuwa Tanzania ni mdau muhimu wa masoko ya kikanda ya EAC, SADC, Soko Huru la Afrika na masoko mengine ya kimataifa.

Mkurugenzi Mkuu wa FCC, William Erio, akizungumza wakati wa kilele cha maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kumlinda Mlaji yaliyofanyika Dar es Salaam.

Naye Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Dk. Eliezer Feleshi, ameshauri elimu iendelee kutolewa kwa umma kuhusu teknolojia hiyo na taasisi zote zishirikishwe ili kuwe na uelewa wa pamoja.

“Akili mnemba ni eneo ambalo linahitaji elimu iendelee kutolewa, lazima taasisi zote zishirikishwe. Tungependa sana wawekezaji, wafanyabiashara na walaji wote tuwe na uelewa wa pamoja,” amesema Jaji Dk. Feleshi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirikisho la Wenye Viwanda Tanzania (CTI), Leodgar Tenga, ameishukuru Tume ya Ushindani Tanzania (FCC) kwa kuelimisha umma kuhusu akili mnemba na kuahidi kuhamasisha matumizi ya teknolojia hiyo kwa wenye viwanda.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa FCC, William Erio, amesema maadhimisho hayo ambayo ni ya 15 tangu Tanzania ianze kuadhimisha mwaka 2009 yamehusisha utoaji elimu kwa umma na wadau mbalimbali kupitia vyombo vya habari kuhusu majukumu ya tume hiyo.

Amesema pia elimu hiyo ilielekezwa katika sekta za uzalishaji, elimu, fedha, afya, Tehama ili kurahisisha utoaji huduma na namna mlaji anavyopaswa kulindwa dhidi ya akili mnemba.


Powered by Blogger.