KAMATI YA BUNGE YAITAKA SERIKALI KUKAMILISHA JENGO LA UTAWALA TIRDO
Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo wakiwa kwenye ziara ya kukagua ujenzi wa jengo la utawala la Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda Tanzania (TIRDO).
Na Nora Damian, The Page
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo imeitaka Wizara ya Viwanda na Biashara kutoa fedha zilizobaki kukamilisha jengo la utawala la Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda Tanzania (TIRDO).
Jengo hilo linajengwa na mkandarasi Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Kujenga Taifa (SUMAJKT) kwa gharama ya Sh bilioni 3.4.
Akizungumza leo Machi 18,2024 wakati wa ziara ya kukagua utekelezaji wa bajeti katika shughuli mbalimbali zinazofanywa na shirika hilo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Deo Mwanyika, amesema jengo hilo limeanza kujengwa miaka mingi hivyo linapaswa kukamilika ili kuendeleza shughuli za utafiti.
“Rais aliidhinisha jengo lililojengwa kwa miaka mingi likamilike, tumekagua tumeridhika wizara imefanya kazi nzuri. Tulipokuja mara ya mwisho hali haikuwa nzuri lakini sasa tunaona ukamilishaji wa jengo ni karibu asilimia 72.
“Serikali ilete fedha zilizobaki kukamilisha jengo hili, tunataka tuone thamani ya kitu kwa kukamilisha mradi,” amesema Mwanyika ambaye pia ni Mbunge wa Njombe Mjini.
Kamati hiyo pia imeishauri Serikali kuliongezea bajeti shirika hilo litekeleze shughuli zake kibiashara na kujitegemea.
“TIRDO ili wasonge mbele wanahitaji wawe na bajeti kubwa zaidi hivyo, wizara ione namna ya kuwasaidia ili wafanye shughuli zao kibiashara wajitegemee,” amesema.
Naye Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Ashatu Kijaji, amesema mpaka sasa fedha zilizopokelewa katika mradi wa jengo hilo ni Sh bilioni 1.54 na zilizobaki zitatolewa katika bajeti ya mwaka 2024/25.
“Kulingana na mkataba mkandarasi anapaswa kukamilisha mradi ifikapo Juni mwaka huu, kwahiyo ataendelea na kazi kisha atawasilisha ‘certificate’ zitakazowezesha kulipa fedha zilizobaki,” amesema Dk. Kijaji.
Waziri huyo amesema pia shirika hilo limekuwa likifanya kazi ya kuvishauri viwanda vinavyotaka kupeleka bidhaa katika Soko Huru la Afrika ambapo mpaka sasa kampuni 11 zimepeleka katika nchi sita.
“Tanzania ni kati ya nchi 54 zilizo katika Soko Huru la Afrika na sisi hatujakwenda kule kama wasindikizaji, Tirdo inavishauri viwanda vyote kuhakikisha yale yanayohitajika katika soko hilo viwanda vinakuwa na uwezo wa kuzalisha katika kiwango kinachokubalika,” amesema.
Meneja Mradi kutoka SUMAJKT, Kanali Saul Chiwanga, amesema ujenzi umefikia asilimia 72 na kuihakikishia kamati hiyo kuwa mradi utakamilika Juni 30,2024.