FCC YAJA NA KLINIKI KUTATUA CHANGAMOTO ZA WALAJI

Mkurugenzi wa Tume ya Ushindani Tanzania (FCC), William Erio, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kumlinda Mlaji.

Na Nora Damian, The Page

Tume ya Ushindani Tanzania (FCC) imewataka Watanzania kujitokeza kwa wingi kuwasilisha kero na changamoto zinazowakabili katika Kliniki ya kusikiliza na kutatua changamoto za mlaji.

Kliniki hiyo ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kumlinda Mlaji iliyoanza kuadhimishwa Machi 8,2024 ambayo inatarajiwa kuhitimishwa Machi 15,2024.

Akizungumza leo Machi 11,2024 wakati wa uzinduzi wa maadhimisho hayo Mkurugenzi wa FCC, William Erio, amesema kliniki hiyo itaendeshwa Machi 13,2024 katika ofisi za FCC Dar es Salaam, Dodoma, Mwanza, Arusha na Mbeya.

“Tunaomba wananchi na wadau wote wasiache kuhudhuria kliniki ya mlaji watapata majibu ya changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo,” amesema Erio.


Kwa mujibu wa Erio, Kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka 2024 inasema; Matumizi ya akili nemba yanayozingatia haki na uwajibikaji kwa mlaji ambayo inasisitiza umuhimu wa kumlinda mlaji dhidi ya athari zinazoweza kujitokeza kutokana na teknolojia hiyo.

“Akili nemba inatumika katika shughuli mbalimbali duniani, ni muhimu kwa sababu na sisi ni sehemu ya dunia hivyo suala hilo haliepukiki,” amesema.

Mkurugenzi huyo amesema pia mlaji ana haki nane na baadhi ya haki hizo ni usalama wa bidhaa na huduma anazopata, haki ya kupata taarifa kuhusu bei, ujazo na malighafi zilizotumika kutengeneza bidhaa mbalimbali.

Amesema kilele cha maadhimisho hayo kitafanyika Machi 15,2024 jijini Dar es Salaam ambapo kutakuwa na kongamano na mada mbalimbali zitatolewa kuhusu akili nemba.


FCC ilianza maadhimisho hayo Machi 8,2024 katika ofisi zake kwa kutoa elimu kupitia redio na mitandao ya kijamii pamoja na semina kwa wadau katika sekta mbalimbali.

Mwaka 1980 Umoja wa Mataifa (UN) ulitengeneza kanuni za kumlinda mlaji na kuanzia mwaka 1983 Siku ya Kumlinda Mlaji imekuwa ikiadhimishwa kila mwaka. Tanzania ilianza kuadhimisha siku hiyo mwaka 2009.







Powered by Blogger.