CHONGOLO ATEULIWA MKUU WA MKOA SONGWE

Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Daniel Chongolo.

Na Nora Damian, Dar es Salaam

Rais Samia Suluhu Hassan amefanya mabadiliko ya wakuu wa mikoa, makatibu tawala, wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa halmashauri ambapo amemteua Daniel Chongolo kuwa Mkuu wa Mkoa wa Songwe.

Chongolo ambaye aliwahi kuwa Katibu Mkuu wa CCM anachukua nafasi ya Dk. Francis Michael.

Aidha aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Ahmed Abbas amehamishiwa Mkoa wa Ruvuma kuchukua nafasi ya Kanali Laban Thomas.

Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa leo Machi 9,2024 na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Dk. Moses Kusiluka, inaeleza kuwa mabadiliko hayo yamelenga kuboresha utendaji kazi wa Serikali.

Wengine waliohamishwa ni aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Tandahimba, Luteni Kanali Patrick Sawala ambaye ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mtwara wakati aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Misungwi, Paul Chacha ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora kuchukua nafasi ya Dk. Batlida Buriani ambaye amehamishiwa Mkoa wa Tanga.

Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Waziri Kindamba ameteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Mabasi Yaendayo Haraka (UDART) ambaye anachukua nafasi ya Gilliard Ngewe ambaye atapangiwa kazi nyingine.

Katika mabadiliko hayo pia aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Halima Dendego, amehamishiwa Mkoa wa Singida kuchukua nafasi ya Peter Serukamba ambaye amehamishiwa Iringa.











Powered by Blogger.