DIWANI MAGRETH CHEKA ATOA MSAADA WA KITI MWENDO
Na Heri Shaaban, Dar es Salaam
Diwani wa Viti Maalum Wilaya ya Ilala, Magreth Cheka ametoa msaada wa kiti mwendo kwa mtoto mwenye ulemavu Leah Ally ili aweze kwenda shule.
Diwani huyo amekabidhi msaada huo Machi 6,2024 katika Kata ya Liwiti wakati wa ziara yake ya kutatua kero ambapo alibaini mtoto Leah (18) amekosa haki ya msingi ya kupata elimu kutokana na kutokuwa na kiti mwendo.
"Nilifanya ziara ya kutembelea Tawi la Umoja wanawake UWT Liwiti Misewe nikapokea changamoto ya Leah, alikuwa akihitaji kiti mwendo ili aweze kwenda shule na nimetekeleza ahadi yangu," amesema Magreth.
Amemtaka mzazi wa Leah kwenda kufuatilia shule ili mtoto huyo aweze kupata elimu kama wengine na kuwaomba wananchi wengine kuunga mkono juhudi zake katika kumsaidia mtoto huyo ambaye anaishi Tabata Liwiti.
Amesema Rais Samia Suluhu Hassan amewekeza katika sekta ya elimu kwa kuboresha miundombinu ya shule za msingi na sekondari ili jamii iweze kupata elimu.
Ametumia fursa hiyo kumpongeza Rais Samia kwa kutekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa vitendo na kuongeza fursa mbalimbali za maendeleo katika nchi.
