UWT NJOMBE WAWAKUMBUKA WATOTO WANAOISHI MAZINGIRA MAGUMU, WAZEE WAKIADHIMISHA SIKU YA WANAWAKE

Mwenyekiti wa UWT Mkoa wa Njombe, Scholastica Kevela, akizungumza na mmoja wa wanafunzi wanaosoma katika Shule ya Msingi Uhenga baada ya kuwapatia misaada mbalimbali.

Na Mwandishi Wetu, Njombe

Baadhi ya wanafunzi wanaoishi kwenye mazingira magumu wanaosoma katika Shule ya Msingi Uhenga Wilaya ya Wanging’ombe mkoani Njombe wamepatiwa sare za shule na mahitaji mengine muhimu ili waweze kuhudhuria masomo vizuri.

Misaada hiyo imetolewa Machi 7,2024 kwa ushirikiano wa Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT) Mkoa wa Njombe na UWT Wilaya ya Wanging’ombe katika kusherehekea Siku ya Wanawake Duniani iliyoadhimishwa kiwilaya katika Kata ya Uhenga.

Mwenyekiti wa UWT Mkoa wa Njombe, Scholastica Kevela, amesema wao ni walezi ndiyo maana wameguswa kuwanunulia mahitaji hayo muhimu ili kupunguza changamoto wanazokutana nazo.

Mwenyekiti wa UWT Mkoa wa Njombe, Scholastica Kevela, akiwa na wazee mbalimbali wakati wa kusherehekea Siku ya Wanawake Duniani iliyoadhimishwa kiwilaya katika Kata ya Uhenga mkoani humo.

"Tunatambua jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan katika kuendeleza sekta ya elimu, na sisi tumeona tutumie siku hii muhimu kumuunga mkono kwa kuangalia makundi muhimu kama ya watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu na wazee,” amesema Kevela.

Amesema pia jamii ina wajibu wa kuwatunza wazee na kuwataka vijana na wanawake wenye uwezo kuliangalia kundi hilo muhimu badala ya kuwaacha wakihangaika.

Wanafunzi waliopatiwa misaada hiyo wameshukuru umoja huo na kuahidi kusoma kwa bidii ili kutimiza ndoto zao na kuwasaidia wazazi wao baadaye.

Baadhi ya madiwani wa viti maalumu waliohudhuria hafla hiyo wamewahimiza wanawake kuzingatia lishe bora ili kuondoa tatizo la udumavu linaloikabili wilaya hiyo na Mkoa wa Njombe.

Kwa upande wao wanawake wa Kata ya Uhenga wameishukuru Serikali kwa jitihada za kuwakwamua kiuchumi ambapo vikundi saba vimenufaika huku kimoja kikipata mradi wa ufugaji kuku 700 kutoka shirika la kuhifadhi mazingira na kurejesha uoto wa asili.

Kaulimbiu ya maadhimisho ya Siku ya Wanawake 2024 inasema; Wekeza kwa wanawake kuharakisha maendeleo ya taifa na ustawi wa jamii.




Powered by Blogger.