NYUMBA YA MTOTO WA MBOWE YAKAMATWA


Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam


Dalali aliyeteuliwa na Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi amekamata nyumba ya Mkurugenzi wa Gazeti la Tanzania Daima, Dudley Mbowe ambaye anadaiwa na waandishi wa gazeti hilo Sh milioni 62.7.

Dalali huyo kutoka Kampuni ya Udalali ya MM Auctioneer & Debt Collectors, Jesca Massawe, leo Februari 28,2024 alifika katika nyumba hiyo iliyopo Mtaa wa Feza Mikocheni A na kubandika matangazo ya kuikamata.

Hatua hiyo ni utekelezaji wa amri ya Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi iliyotolewa Februari 13,2024.

Hata hivyo Dudley alionekana kutoridhishwa na utaratibu huo na kuomba matangazo yasibandikwe lakini dalali alikataa na kubandika katika maeneo mbalimbali ya nyumba hiyo.


Muda mfupi baada ya kubandikwa matangazo hayo Dudley alisikika akisema uamuzi huo utawagharimu walalamikaji kwa kuwa umechukuliwa kisiasa kisha alionekana akiyabandua ingawa dalali alimwambia haruhusiwi kufanya hivyo kwa mujibu wa maagizo ya Mahakama Kuu.

Februari 13,2024 Mahakama hiyo ilitoa amri na kumteua dalali wa kukamata nyumba hiyo kwa lengo la kuipiga mnada kwa kushindwa kulipa Sh milioni 62.7 za waandishi wa habari.

Uamuzi huo ulitolewa mbele ya Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Mary Mrio, baada ya kupitia hoja za washinda tuzo katika Tume la Usuluhishi na Uamuzi (CMA) Julai 2023.

Shauri hilo namba 28461 la mwaka 2023, wadai ni Maregesi Paul na wenzake tisa dhidi ya Mkurugenzi wa Gazeti la Tanzania Daima, Dudley Mbowe.

Awali ilidaiwa mahakamani kuwa baada ya wadai kushinda shauri Dudley alikubali kulipa lakini hakutekeleza makubaliano hivyo wadai waliona njia sahihi ni kukamata nyumba yake.

Naibu Msajili Mrio alitoa amri ya kukamata nyumba namba tisa, iliyopo Mtaa wa Feza, Mikocheni.

Shauri hilo litatajwa tena Machi 4 mwaka huu kwa ajili ya kupata taarifa ya utekelezaji wa amri hiyo.

Walalamikaji walipata tuzo Julai 17,2023 mbele ya Mwenyekiti wa CMA, Bonasia Mollel.

Awali walikuwa wanadai Sh milioni 114 lakini baada ya kukaa kwenye majadiliano kwa pamoja kiwango hicho cha fedha kilishuka na kufikia Sh milioni 62.7.

Dudley alikubali kulipa fedha hizo kwa awamu tatu; Oktoba 30, Desemba 30,2023 na awamu ya mwisho ilikuwa mwishoni Februari,2024.

Desemba 20,2023 Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, aliwaita wahariri wa Gazeti la Tanzania Daima ambao ni miongoni mwa wadai na baada ya majadiliano alikubali kulipa madai ya wafanyakazi hao mwishoni mwa Desemba lakini hajafanya hivyo hadi sasa.
Powered by Blogger.