WANANCHI NARUNG’OMBE – LIKOMA WALALAMIKIA UCHAFUZI WA KELELE


Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Wananchi wa Mtaa wa Narung’ombe na Likoma katika Kata ya Kariakoo wamelalamikia uchafuzi unaotokana na kelele kutoka katika nyumba ya ibada waliyodai kuwa si rasmi.

Wakizungumza Februari 27,2024 na Waandishi wa habari wananchi hao ambao majina yao yanahifadhiwa wamesema wanaheshimu uhuru wa kuabudu lakini wanataka ufanyike kwa kuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa.  

“Hapa mtaani tuna misikiti mitatu ukiwemo wa Idrissa hiyo hatuna tatizo nayo kabisa, ila kuna ambao umeanzishwa hivi karibuni kwenye nyumba ya mtu. Tunapata taabu na wengine tunaumwa kwa sababu kelele zimezidi, tumeshapeleka malalamiko Nemc (Baraza la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira), Bakwata lakini bado hatujapata ufumbuzi,” amesema mmoja wa wananchi hao.

Mwananchi mwingine amesema amekuwa akilazimika kwenda kulala katika nyumba za wageni kutokana na kero ya kelele hizo.

“Nikisema nilale nyumbani kwangu labda nimeze dawa za usingizi kwa sababu unajikuta umekaa macho tu usingizi hauji, ndiyo maana mimi wakati mwingine naamua kwenda kulala ‘guest’,” amesema.

Wananchi hao wameziomba mamlaka zinazohusika kuwasaidia kutatua changamoto hiyo ili waendelee kuishi kwa utulivu. 

Ofisa kutoka Baraza la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Emile amesema tayari waliwaita walalamikiwa hivyo wanaendelea kushughulikia suala hilo kuweza kulipatia ufumbuzi.  

Kulingana na Sheria ya Mazingira 2004 kifungu cha 106 (5) si ruhusa kwa mtu yeyote kupiga kelele au kusababisha kelele kuzidi kiwango kilichoainishwa au kitakachobainishwa kuhusiana na upigaji kelele.

Aidha kifungu kidogo cha (6) cha sheria hiyo kinasema ni kosa kwa mtu yeyote kupiga kelele bila kuzingatia njia iliyobainishwa kuwa ni bora. 



Powered by Blogger.