KIKWETE, LOWASSA NA SIRI YA URAIS
Rais mstaafu, Jakaya Kikwete (kushoto) na Hayati Edward Lowassa.
Na Nora Damian, Dar es Salaam
Siku mbili tangu taifa lipate msiba wa Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa watu mbalimbali wanaendelea kumzungumzia lakini kubwa ni harakati zake za kugombea urais.
Lowassa aliyefariki Februari 10,2024 inaelezwa kuwa alianza harakati za kusaka urais mwaka 1995 na licha ya kutofanikiwa alijaribu tena mwaka 2015.
Rais mstaafu, Jakaya Kikwete, leo Februari 12,2024 ameeleza namna walivyoanza safari ya urais wakiwa na Lowassa.
Kikwete ambaye alifika nyumbani kwa Lowassa Masaki Dar es Salaam na kutoa pole pia alitumia nafasi hiyo kumzungumzia kiongozi huyo.
Rais mstaafu, Jakaya Kikwete, akisaini kitabu cha maombolezo katiba msiba wa Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, Masaki Dar es Salaam.
“Siku moja nikiwa nyumbani nikapokea ugeni, mtoto akaja chumbani akaniambia baba kuna wageni, nikaenda nikakuta marafiki zangu watatu. Kaka yangu Samuel Sitta (aliyewahi kuwa Spika wa Bunge), Edward Lowassa na Rostam Aziz.
“Msemaji alikuwa Samuel Sitta, wakaja kuniambia kwamba tunataka muende na Edward Dodoma mkachukue fomu ya kugombea urais mwaka 1995. Mimi nikasema jambo hilo halipo kwenye mawazo yangu, lakini mwenzangu yeye lipo kwenye mawazo yake basi muacheni aende…yeye akasema siendi bila wewe.
“Tulibishana mpaka tukafika mahali tukakubaliana basi acha twende, mchakato wa ndani ya chama mwenzangu hakubahatika, mimi nikabahatika kuwemo katika wale watano.
“Baadaye tukapiga kura kwenye NEC nikawemo katika wale watatu, kwenye mkutano mkuu nikawemo katika wawili lakini kura zangu hazikutosha akapata Mzee Mkapa,” amesema Kikwete.
Amesema Lowassa ametoa mchango mkubwa katika taifa na kwamba yalitokea ni changamoto katika maisha lakini hayafuti mema na mazuri aliyoyafanya.
“Mwezangu aliteuliwa kuwa waziri mkuu, akapata changamoto ikabidi akae pembeni, tuliendelea kuwa pamoja, kuwa marafiki tukishirikiana kwa kila linalowezekana.
“Ninachoshauri tuendelee kumuombea kwa mwenyezi Mungu aipumzishe roho yake, ametoa mchango mkubwa katika taifa, yalitokea ni changamoto katika maisha lakini hayafuti mema na mazuri aliyoyafanya taifa letu,” amesema Kikwete.
Lowassa ambaye alitumikia Serikali kwa miaka 35 katika nafasi mbalimbali alifariki Februari 10,2024 katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) alikokuwa akipatiwa matibabu na anatarajiwa kuzikwa Februari 17,2024 nyumbani kwake Monduli mkoani Arusha.

