‘BONNAH ANAFAA 2025 AACHWE AFANYE KAZI’
Na Nora Damian, Dar es Salaam
Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, Anamringi Macha amesema katika Jimbo la Segerea kuna ushirikishwaji mkubwa kati ya mbunge na madiwani hatua inayorahisisha utekelezaji Ilani ya Uchaguzi.
Amesema katika baadhi ya maeneo kuna mgawanyiko ambapo baadhi ya madiwani wamekuwa hawashirikiani na wabunge licha ya kwamba wote dhamana zao zinafanana lakini hali ni tofauti katika Jimbo la Segerea.
Macha ameyasema hayo Februari 11,2024 wakati wa mkutano mkuu maalumu wa Jimbo la Segerea ambapo Mbunge Bonnah Kamoli aliwasilisha utekelezaji wa Ilani ya CCM na mafanikio ya miaka mitatu ya Rais Samia katika jimbo hilo.
“Lazima niwe mkweli kwa Segerea kuna ushirikishwaji mkubwa na wa kiwango cha juu kati ya mbunge na madiwani, huu ni mfano wa kuigwa. Mtu mmoja angeniuliza kikosi hiki (mbunge na madiwani) ningesema kinafaa kwa 2025.
“Mheshimiwa mbunge na madiwani sina nia yoyote ya kuwapigia kampeni lakini mtu anayetekeleza majukumu yake kwa ufanisi tusiogope kumsifu…msim - distable mbunge, mmuache bado anafaa na anatosha,” amesema Macha.
Wajumbe wa mkutano mkuu maalumu wa Jimbo la Segerea wakifuatilia utekelezaji wa Ilani ya CCM katika jimbo hilo.
Katika mkutano huo Macha amesema ameridhishwa na kazi zilizofanywa katika jimbo hilo na kwamba Bonnah amekuwa daraja zuri la kuunganisha Serikali kuu na jimbo na kuhakikisha juhudi zinazofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan zinaeleweka vizuri kwa wananchi.
Katika mkutano huo Bonnah aliwasilisha utekelezaji ilani kielektroniki kwa kuonyesha mambo yaliyofanyika katika kata zote 13 za jimbo hilo kupitia video.
“Lazima nikiri hii ‘documentary’ imenifupishia kazi, mwenye macho haambiwi tazama, tulizoea taarifa za kusomeana lakini mbunge ametuonyesha taarifa hizo mubashara.
“Bonnah angeweza kutumia dakika 40 au zaidi kutoa maelezo badala yake amewaachia wenzake (madiwani) waeleze yaliyotekelezwa kwenye kata zao. Ana uhakika, hana mashaka na watu alionao na haya ndiyo mahusiano tunayotaka ya utendaji kazi,” amesema.
Naibu Katibu Mkuu huyo pia amewatahadharisha watendaji wa chama na Serikali kuacha kupanga safu za wagombea badala yake wazingatie kanuni na taratibu.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Ilala, Said Sidde, amesema; “Bonnah ni miongoni mwa wabunge wachache na tunu katika wilaya yetu na heshima kubwa kwa chama.


