WAZIRI WA UTALII ZANZIBAR AJIUZULU
Na Mwandishi Wetu
Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Simai Mohamed Said ametangaza kujiuzulu wadhifa huo.
Simai ambaye ni Mwakilishi wa Tunguu kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) ametangaza uamuzi huo Januari 25,2024.
Katika video iliyosambaa mitandaoni Simai amesema amejiuzulu nafasi hiyo kwa kile alichodai kuwa ni kutokuwepo kwa mazingira yasiyo rafiki katika kutekeleza jukumu hilo.
"Usiku huu wa tarehe 25 nimeandika barua rasmi kwenda kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ya kujiuzulu nafasi yangu kuanzia leo.
"Nimefikia uamuzi huu ambao hapa kwetu si rahisi katika utamaduni wetu. Inapotokea mazingira yasiyo rafiki kutekeleza majukumu ni vema kutafuta jawabu la haraka ili kazi ya kuwaletea wananchi maendeleo iweze kuendelea ikibidi kukaa pembeni...mimi nimefikia uamuzi huo mgumu wa kukaa pembeni," amesema Simai katika video hiyo.
Amemshukuru Rais Dk. Hussein Mwinyi kwa kumwamini na kumteua kuwatumikia Wazanzibar na kuahidi kuwa ataendelea kuwa mtiifu kwa Serikali pamoja na chama chake.
