WATAHINIWA 102 WAFUTIWA MATOKEO KWA UDANGANYIFU
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA) limefuta matokeo ya watahiniwa 102 kwa kufanya udanganyifu ikiwemo kuandika matusi kwenye karatasi za majibu.
Akitangaza matokeo hayo leo Januari 25,2024 Katibu Mtendaji wa NECTA, Dk. Said Mohamed, amesema watahiniwa 572,359 walisajiliwa kufanya mtihani
huo Novemba mwaka 2023.
Amesema watahiniwa watano wamefutiwa matokeo kwa kuandika lugha ya matusi.
Aidha baraza hilo limezuia kutoa matokeo ya watahiniwa 376 ambao walipata matatizo ya kiafya na kushindwa kufanya mtihani kwa masomo yote au idadi kubwa ya masomo.
Amesema jumla ya watahiniwa 484,823 sawa na asilimia 87.65 ya watahiniwa waliofanya Mtihani wa Kidato cha nne mwaka jana wamefaulu.
Amesema kati yao wasichana ni 257,892 sawa na asilimia 86.17 huku wavulana wakiwa 226,931 sawa na asilimia 89.40.
Kuhusu watahiniwa wa kujitegemea amesema waliofaulu ni 13,396 sawa na asilimia 52.44.
Amesema ubora wa ufaulu unaonesha watahiniwa waliopata ufaulu mzuri wa daraja la kwanza hadi la tatu ni 197,426 sawa na asilimia 37.42.
Katibu Mtendaji huyo amesema ubora wa ufaulu wa daraja la kwanza hadi tatu ni mzuri zaidi kwa wavulana ikilinganishwa na wasichana ambapo wavulana ni 108,368 sawa na asilimia 44.47 na wasichana ni 89,058 sawa na asilimia 31.37.
