WATU 500 WAPATIWA HUDUMA JKCI GEITA, 22 WAPEWA RUFAA


Wakazi wa Mkoa wa Geita wakisubiri kupatiwa huduma katika kliniki maalumu ya Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete iliyopo katika Maonyesho ya Sita ya Kimataifa ya Teknolojia ya Madini yanayofanyika viwanja vya EPZA mkoani Geita. (Picha na Nora Damian).

Na Nora Damian, Geita

Watu 290 kati ya 500 wamebainika kuwa na matatizo mbalimbali ya moyo huku 22 wakipewa rufaa kwenda Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) kwa uchunguzi zaidi.

Taasisi hiyo imeweka kliniki maalumu katika Maonyesho ya Sita ya Kimataifa ya Teknolojia ya Madini yanayofanyika viwanja vya EPZA mkoani Geita ambapo wanafanya uchunguzi wa awali wa maradhi ya moyo, sukari pamoja na kupima uzito na urefu.

Akizungumza na waandishi wa habari Septemba 26,2023 Daktari Bingwa wa Moyo JKCI, Saleh Mwinchete, amesema kwa siku wanahudumia wastani wa watu 100 na kati yao 30 hubainika kuwa na presha.

“Tumeona watu wengi wana shida ya presha na hawafahamu kama wanayo, ni maradhi ambayo hayana dalili kwa asilimia kubwa…asilimia 90 mpaka 95 mtu anaweza asisikie chochote akawa mzima anaendelea na shughuli zake.

“Katika watu 10 ambao wana maradhi ya presha wanane hawajui chochote, hawana dalili. Tumetumia fursa hii kuwaelimisha, kuwaanzishia dawa na kuwaambia namna bora ya kuishi ili kujilinda na maradhi ya presha,” amesema Dk. Mwinchete.

Daktari Bingwa wa Moyo JKCI, Saleh Mwinchete, akimpima mkazi wa Geita aliyejitokeza kupatiwa huduma katika kliniki maalumu ya taasisi hiyo iliyopo katika Maonyesho ya Sita ya Kimataifa ya Teknolojia ya Madini yanayofanyika viwanja vya EPZA mkoani Geita. (Picha na Nora Damian).

Amesema wanatoa elimu kwa wananchi na washiriki wengine wa maonyesho hayo waweze kufahamu visababishi vya maradhi ya moyo.

“Tumeona watu ambao uzito wao ni mkubwa kuliko uwiano wa urefu, watu ambao wana maradhi ya presha, magonjwa mbalimbali ya moyo mfano matundu kwenye moyo,” amesema Dk. Mwinchete.

Daktari huyo ameishauri jamii kuishi maisha rafiki kwa afya ya moyo kwa kufanya mazoezi, kupunguza ulaji chumvi, kuepuka unywaji pombe usiofaa na ikibidi kuacha, kupunguza uzito, kutovuta sigara na kutojipa msongo wa mawazo.

“Tunawaomba wananchi wawe na utamaduni wa kujichunguza, kuna maradhi ambayo hayatakupa dalili yoyote lakini yakawa na athari kubwa katika mwili…presha isipotibiwa unaweza kupata kiharusi na upungufu wa nguvu za kiume,” amesema Dk. Mwinchete.

Baadhi ya wakazi wa Mkoa wa Geita waliopatiwa huduma wameishukuru taasisi hiyo na kuiomba iendelee kutoa huduma za kibingwa katika hospitali za mkoa huo.

“Niliposikia Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete wapo kwenye maonyesho nilifurahi sana kwa sababu wametusogezea huduma, kama ningetakiwa kwenda kuifuata Dar es Salaam ingenigharimu,” amesema Anastazia Costantine (71) mkazi wa Geita.














Powered by Blogger.