WATANZANIA CHANGAMKIENI FURSA ZA UWEKEZAJI GEITA – KINGALAME
Mkuu wa Wilaya ya Nyang'wale, Grace Kingalame, akizungumza wakati wa kongamano la wadau wa sekta ya madini kujadili fursa za uwekezaji zilizopo mkoani Geita.
Na Nora Damian, Geita
Watanzania wametakiwa kujitokeza kuchangamkia fursa za uwekezaji zilizopo katika Mkoa wa Geita na kuwekeza katika sekta mbalimbali kama vile madini, viwanda na kilimo.
Oktoba 2022 Rais Samia Suluhu Hassan alisema wanalenga kuufanya Mkoa wa Geita kuwa kitovu cha uchumi katika Ukanda wa Afrika Mashariki kwa kuwa umekaa vizuri kiuchumi.
Viongozi mbalimbali wameendelea kutangaza fursa za biashara na uwekezaji zilizopo katika mkoa huo huku wakiwahakikishia mazingira bora wawekezaji.
Leo Septemba 26,2023 Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Geita ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Nyang’wale, Grace Kingalame, ametumia kongamano la uwekezaji kwa wadau wa sekta ya madini kutangaza fursa zilizopo mkoani humo.
Kongamano hilo limeshirikisha washiriki wa Maonyesho ya Sita ya Kimataifa ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea katika viwanja vya EPZA Bombambili mkoani Geita.
Kingalame amezitaja baadhi ya fursa hizo kuwa ni katika sekta ya madini, utalii (Hifadhi za Taifa za Burigi – Chato, Rubondo), Soko la Kimataifa la Samaki, vyuo na taasisi za elimu ya juu,
“Mheshimiwa Rais Samia anaendelea kuweka mazingira bora ya uwekezaji ambayo yamewafanya wawekezaji wengi waendelee kuja Geita, tunawakaribisha na tunawahakikishia mazingira bora ya uwekezaji na na hakutakuwa na bugudha katika kufanya shughuli zao.
“Wana – Geita tuendelee kuchangamka kuhakikisha tunapata wawekezaji na kuendelea kukua kiuchumi,” amesema Kingalame.
Amesema mbali ya dhahabu mkoa huo unafanya vizuri katika sekta ya kilimo na ufugaji ambazo zimetoa ajira rasmi na zisizo rasmi kutokana na uwekezaji unaofanywa.
Akizungumzia Wilaya ya Nyang’wale amewahakikishia wawekezaji kwamba hawatapata taabu kuwekeza kwa kuwa tayari wameandaa mazingira mazuri.
“Wilaya ya Nyang’wale imebarikiwa, wengine wakisikia jina wanaogopa, mimi nilivyofika Nyang’wale kwa mara ya kwanza nililala usiku nikamwambia Mungu kwanini umenichelewesha kufika Nyang’wale.
“Nyang’wale imebarikiwa kuwa na madini, tuna wachimbaji wengi, ni wilaya ambayo inatoa mchele bora, tunalima sana matikiti maji, mnaweza kuja kuwekeza katika sekta ya viwanda vya kuchakata mpunga…karibuni Nyang’wale nawahakikishia usalama wenu ndio kipaumbele chetu.
“Tutamsaidia Rais Samia kuhakikisha Geita inakwenda mbele na Tanzania inakuwa kinara kama ambavyo ametuheshimisha kwenye suala zima la diplomasia, ndio maana wawekezaji wengi wanakimbilia Tanzania kwa sababu ya mazingira bora ya uwekezaji aliyoyaweka,” amesema Kingalame.

