MAAGIZO YA AWESO KWA BODI ZA MAJI

Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, akizungumza wakati wa mafunzo kwa wakurugenzi na menejimenti za mamlaka za majisafi na usafi wa mazingira, jijini Dar es Salaam.

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amezindua Bodi za Mamlaka za Maji nchini na kuwataka viongozi kushirikiana na wadau wengine katika sekta hiyo kuhakikisha inasonga mbele.

Waziri Aweso ameyasema hayo Septemba 25,2023 wakati akifungua kikao cha mafunzo kwa wakurugenzi na menejimenti za mamlaka za majisafi na usafi wa mazingira, jijini Dar es Salaam.

Amemtaka Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Profesa Jamal Katundu, kuhakikisha bodi hizo zinapokea maoni kisha kutoa majibu kwa makundi mbalimbali wakiwemo viongozi wa kisiasa, Serikali, wafanyabiashara na watumishi wastaafu waliobobea katika masuala ya maji.

"Hatuwezi kufanya kazi peke yetu, lazima tuhakikishe tunashirikiana na wadau wengine ili kuhakikisha tunafikia malengo tuliyojiwekea.

"Lengo ni kufikia upatikanaji wa huduma ya maji vijijini kwa asilimia 85 na mijini asilimia 95 na kupita kiwango hicho ili kuwafikia wananchi na kumtua mama ndoo ya maji kichwani," amesema Aweso.

Amesema hivi sasa zoezi la utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maji linaendelea vizuri na kusisitiza utoaji huduma za uhakika na taarifa kwa wateja pale inapotokea hitilafu katika uzalishaji.


Akizungumzia suala la upotevu wa maji (NRW) amezitaka bodi kufuatilia kwa kina mivujo na kiwango cha maji kinachopotea ili kuona uhalisia wa maji na kutoa taarifa kwa sababu yanaweze kutumika bila kulipiwa.

Mafunzo hayo yameshuhudia bodi za wakurugenzi za mamlaka za maji 25 zikizinduliwa na baadhi ya mamlaka za maji zikipandishwa madaraja kuendana na vigezo ikiwamo vya utoaji huduma na kumudu kujiendesha.






Powered by Blogger.