CRDB YAJIVUNIA KUKOPESHA WACHIMBAJI IKISEMA NI WALIPAJI WAZURI

Meneja wa Biashara wa CRDB Kanda ya Magharibi, Anselem Mwenda, akizungumza wakati wa kongamano la wadau wa sekta ya madini wanaoshiriki Maonyesho ya Sita ya Kimataifa ya Teknolojia ya Madini katika viwanja vya EPZA Bombambili, mkoani Geita.

Na Nora Damian, Geita

Benki ya Crdb imetoa mikopo mbalimbali kwa wachimbaji wadogo, wa kati na wakubwa na kusema mpaka sasa hawajakutana na tatizo lolote kwa wakopaji husika.

Akizungumza Septemba 25,2023 Meneja wa Biashara wa CRDB Kanda ya Magharibi, Anselem Mwenda, amesema wamebuni huduma maalumu katika kanda hiyo ili kuongeza ufanisi katika shughuli za wachimbaji.

Meneja huyo alikuwa akizungumza wakati wa kongamano la wadau wa sekta ya madini wanaoshiriki Maonyesho ya Sita ya Kimataifa ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea katika viwanja vya EPZA Bombambili mkoani Geita.

Kwa mujibu wa Meneja huyo, huduma hiyo imeanza kutolewa kwa mfano katika maeneo ya Nyang’wale, Mbogwe na Kakola mkoani Geita.

“Tunakopesha wachimbaji wadogo kabisa na tayari wapo ambao wameshanufaika na mikopo, mpaka sasa hatujakutana na tatizo lolote kwenye mikopo ya wachimbaji wadogo…mmeonyesha ni walipaji wazuri.

“Sisi kama benki tunaamini pamoja na kwamba tumeanza kama ‘pilot’ katika maeneo hayo lakini tutaendelea kwenda kwenye maeneo yote ambayo yana rasilimali ya madini,” amesema Mwenda.


Aidha amesema wanakopesha wachimbaji wa kati na wakubwa na tayari wengine wamefanikiwa kupata mashine kubwa za kuchimba dhahabu.

Kwa mujibu wa Meneja huyo, mikopo kama hiyo imetolewa katika Wilaya ya Nyang’wale, Kahama na nyingine na kwamba haina masharti magumu.

“Kuna mikopo ambayo tunaitoa waombaji hawalazimiki kuweka dhamana za ziada, kama ni mashine au ‘truck’ au mitambo inasimama kama dhamana,” amesema Mwenda.

Naye Meneja wa Benki ya CRDB Geita, Efrosina Mwanja, akizungumza wakati wa ufunguzi wa ofisi za Kampuni ya GF Trucks and Equipment mkoani humo, amesema wanashirikiana na kampuni hiyo kuwakopesha wachimbaji magari na vifaa.

“Tunawakopesha Watanzania, mfanyabiashara au mchimbaji, atachangia asilimia 30 ya gharama ya manunuzi ya gari au vifaa. Kwahiyo tunatoa asilimia 70 ya gharama zote na dhamana ni chombo alichonunua,” amesema Mwanja.

Amesema pia wamekuwa wakiwapeleka wachimbaji wadogo nje kama vile China, Dubai na Uturuki kwa lengo la kujifunza na kuongeza ufanisi katika shughuli za madini.

Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika matukio hayo amepongeza jitihada zinazofanywa na Crdb akisema watatumia mbinu za benki hiyo katika maeneo mengine ili kuwawezesha wachimbaji kupata mitaji kirahisi.

Katika maonyesho hayo benki hiyo inatoa elimu kwa washiriki kuhusu huduma mbalimbali walizonazo ikiwemo pia vigezo na masharti ya mikopo kwa wachimbaji.











Powered by Blogger.