'UKIWA NA MILIONI 50 UNAJENGA KITUO CHA MAFUTA'
Meneja wa Ewura Kanda ya Ziwa, George Mhina, akizungumza wakati wa kongamano la wadau wa sekta ya madini lililofanyika katika Maonyesho ya Sita ya Teknolojia ya Madini yanayofanyika viwanja vya EPZA mkoani Geita.
Na Nora Damian, Geita
Mamlakala ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) imewahamasisha wafanyabiashara kujenga vituo vya mafuta katika maeneo ya vijijini ili kurahisisha upatikanaji wa nishati hiyo.
Mamlaka hiyo imerahisisha mifumo ya kuomba leseni kwa vituo vya vijijini ambapo gharama ni Sh 50,000 na ada kwa miaka mitano ni Sh 500,000.
Akizungumza Septemba 22,2023 Meneja wa Ewura Kanda ya Ziwa, George Mhina, amesema wametengeneza kanuni mahususi na kuondoa masharti magumu ya ujenzi wa vituo vya mafuta.
Meneja huyo alikuwa akizungumza wakati wa kongamano la wadau wa sekta ya madini lililofanyika katika Maonyesho ya Sita ya Teknolojia ya Madini yanayofanyika viwanja vya EPZA mkoani Geita.
“Wakati mwingine mtu anaweza kutembea umbali mrefu bila kukuta kituo cha mafuta, kwahiyo tumetengeneza kanuni mahususi na kuondoa yale masharti magumu ya ujenzi wa vituo vya mafuta.
“Ukiwa na shilingi milioni 50 tu unaweza kujenga kituo cha mafuta kijijini na ukatoa huduma kwahiyo tuchangamkie fursa,” amesema Mhina.
Kulingana na mamlaka hiyo ujenzi wa vituo katika maeneo ya mjini huweza kugharimu kati ya Sh milioni 300 hadi 500 lakini kwa vijijini gharama ni nafuu.
Meneja hayo amesema mifumo ya kuomba leseni inafanyika kidijitali ambapo mtu anaweza kuomba akiwa mahali popote.
Amesema pia wametengeneza kanuni mahususi za kushughulikia malalamiko na kutoa wito kwa wananchi wenye malalamiko mbalimbali kuhusiana na huduma za maji na umeme kuyawasilisha.
“Mfano kama uliomba kuunganishiwa umeme halafu mtoa huduma akachukua fedha zako imepita miezi miwili au mitatu hujaunganishiwa unaweza kuleta malamamiko kwetu.
“Umeletewa bili ya maji au ya umeme ukawa hujaridhika nayo unaweza kuleta malalamiko kwetu,” amesema.
Aidha amesema katika mwaka huu wa fedha (2023/24) wameanzisha kanda mpya ya Magharibi kwa lengo la kusogeza huduma karibu na wananchi.
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika kongamano hilo amesema mazingira bora ya ufanyaji biashara Tanzania yanawezekana na kuwataka wachimbaji kujitahidi kujua na kuelewa taratibu za namna ya kupata leseni na huduma mbalimbali zinazotolewa na taasisi za umma.
“Sisi kama Serikali kupitia taasisi hizi tuna kazi ya ziada ya kuhakikisha tunaendelea kutoa elimu ya jinsi ambavyo tunatakiwa kuwahudumia Watanzania katika seta zote hasa sekta ya madini.
“Majukumu yawe ni kuwasaidia, suala la kwamba amekosea tusingependa kuona wanakosea, tuwaambie taratibu na kanuni za ufanyaji biashara mbalimbali. Tuhakikishe tunaendelea kuwapa elimu wajue taratibu, kanuni na sheria ili tusifike sehemu ya kuwapa adhabu.
“Changamoto kubwa ni elimu, Watanzania wengi sasa wameamka, wachimbaji wadogo mchango wao ni mkubwa kwahiyo ni vema tuhakikishe tunawasaidia wawe wa kati na baadaye wawe wakubwa, tusipowalea tutaendelea kuona makampuni makubwa ya nje,” amesema Kigahe.
