RAIS MWINYI: SEKTA YA BIMA NI MUHIMU KWA UCHUMI
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi akizungumza na ujumbe wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania, Ikulu Zanzibar.
Na Mwandishi Maalumu, Zanzibar
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema anatambua umuhimu wa mchango wa sekta ya bima kwa uchumi wa nchi na kujikinga dhidi ya majanga mbalimbali.
Rais Mwinyi ameyasema hayo leo Septemba 4, 2023 alipokutana na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), Dk. Baghayo Saqware na ujumbe wake waliofika Ikulu Zanzibar.
Aidha, Dk. Mwinyi amepongeza juhudi zinazofanywa na mamlaka hiyo kwa kuanzisha konsotia ya kilimo na kuwataka kupanua wigo zaidi katika sekta za mifugo na uvuvi kwa kugusa wananchi wengi zaidi.
Naye Kamishna Saqware amewatambulisha Mabalozi wa Mamlaka hiyo kwa Rais Mwinyi akiwemo Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Injinia Zena Ahmed Said na Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Wanu Hafidh Ameir na Japhet Hasunga ambao moja ya majukumu yao ni kutoa elimu ya uelewa wa bima kwa wananchi.


