AWESO ASISITIZA UTATUZI CHANGAMOTO SEKTA YA MAJI KWA WAKATI



Na Mwandishi Wetu, Dodoma


Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, amewataka watumishi wa Sekta ya Maji kuhakikisha wanatatua changamoto za sekta hiyo kwa haraka na kwa wakati.

Ametoa agizo hilo leo Septemba 4, 2023 jijini Dodoma katika kikao kazi kilichowakutanisha watendaji na watumishi wa taasisi zilizoko chini ya wizara hiyo.

Amesema lengo la Wizara ya Maji ni kuhakikisha inaendelea kuwa wizara bora kwa kutoa huduma ya maji kwa wanachi ili kuleta maendeleo nchini.

“Niwatake wote mkatekeleze majukumu yenu, mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ametuamini na kuendelea kutuweka pamoja katika wizara hii, hivyo tushirikiane tukafanye kazi ili kuhakikisha malengo yetu yanafikiwa," amesema Aweso.
Waziri wa Maji, Jumaa Aweso.

Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Maryprisca Mahundi, amesema weledi na kasi katika utekelezaji wa miradi ya maji unatoa mwanga na mwelekeo mzuri katika kila kona ya nchi, hivyo juhudi hizo ziendelee na kuwashirikisha wananchi kwani ndio wanufaika wakubwa na wadau wa Serikali katika miradi ya maji.

Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Profesa Jamal Katundu, aliyeteuliwa hivi karibuni ameahidi kuwa kiongozi wa kusukuma maendeleo mbele zaidi ili kufikia malengo ya nchi.

Amesema kushirikiana na kutatua changamoto kwa pamoja kutahakikisha huduma ya maji kwa kila Mtanzania inatimia kwa wakati na ziada pia kwa kufikisha maji vijijini kwa silimia 85 na mijini kwa asilimia 95.

“Kila mmoja katika nafasi yake ahakikishe analenga kwenda zaidi ya hapo," amesema Profesa Katundu.

Naye Naibu Katibu Mkuu, Mhandisi Mwajuma Juma, amesema maendeleo yote yaliyopatikana katika Sekta ya Maji yamebebwa na ushirikiano wa dhati kati ya watumishi na viongozi.

Mhandisi Mwajuma ambaye naye ameteuliwa hivi karibuni ameahidi kutoa ushirikiano kuhakikisha Watanzania wanapata majibu ya uhakika kuhusu huduma ya maji ambayo inakuwa endelevu katika makazi yao.
Powered by Blogger.