NYUNDO TANO ZA MAVUNDE KWA WACHIMBAJI

Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, akizungumza wakati wa ufunguzi wa Maonyesho ya Sita ya Kimataifa ya Teknolojia ya Madini  viwanja vya EPZA mkoani Geita.

Na Nora Damian, Geita

Dakika 10 za Waziri wa Madini, Anthony Mavunde zilitosha kukonga mioyo ya wachimbaji kutokana na mikakati aliyoieleza ya kuendeleza sekta hiyo nchini.

Wachimbaji walikuwa wakimsikiliza Mavunde wakati wa ufunguzi wa Maonyesho ya Sita ya Kimataifa ya Teknolojia ya Madini yanayofanyika viwanja vya EPZA mkoani Geita ambayo yalifunguliwa Septemba 23,2023.

Mavunde alikuwa mzungumzaji wa 14 aliyeanza saa 11:38 jioni hadi saa 11:48 jioni kisha kumkaribisha Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko ambaye alikuwa mgeni rasmi.

Mavunde alitaja mambo matano muhimu atakayoyasimamia; kuhakikisha mchango wa sekta ya madini katika Pato la Taifa unafikia asilimia 10 ifikapo 2025, kupima eneo lote Tanzania ili kujua lenye madini, upatikanaji wa mitaji kwa wachimbaji, kushughulikia migogoro na kudhibiti utoroshwaji wa madini.

Amesema mwaka 2021 sekta hiyo ilikuwa inachangia asilimia 7.7 ya Pato la Taifa na kwa sasa inachangia asilimia 9.8.

“Kabla ya mwaka 2025 haujafika tunataka lengo kuu litimie, hii siyo kazi ndogo, nataka nikuahidi (Dk. Biteko) kwamba nitasimamia hapo hapo, nitaweka mguu chini ili nchi yetu inufaike na madini ambayo Mwenyezi Mungu ametujalia,” amesema Mavunde.

Waziri wa Madini, Anthony Mavunde.

Amesema sekta hiyo inachangia asilimia 56 za fedha za kigeni na imekuwa ikiongoza katika sekta zote wakati katika mapato ya kodi ya ndani ikichangia asilimia 15 sawa na Sh trilioni 2.

“Nimekuja na Vision 2030, madini ni maisha na utajiri tunataka ikifika mwaka 2030 tuwe tumepata taarifa ya kijiolojia ya nchi yetu eneo lote lililobaki,” amesema.

Kwa mujibu wa Mavunde eneo lenye taarifa ambazo zimefanyiwa utafiti wa kina kwa sasa ni asilimia 16.

Aidha amesema wapo kwenye mchakato wa kuanzisha benki ya wachimbaji wadogo itakayowasaidia kupata mitaji na mikopo ya uhakika.

“Nimemuelekeza mkurugenzi wa Stamico (Shirika la Madini) akutane na mabenki yote Tanzania tufanye mkutano wa pamoja tujue changamoto gani mabenki wanazo washindwe kuwakopesha wachimbaji.

“Wachimbaji wenyewe kwa wenyewe wanakopeshana mpaka shilingi bilioni moja na wanazisimamia zinarudi kwanini mabenki washindwe kuwakopesha?” amehoji Mavunde.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko, akizungumza wakati wa ufunguzi wa Maonyesho ya Sita ya Kimataifa ya Teknolojia ya Madini  viwanja vya EPZA mkoani Geita.

Waziri Mavunde pia amewatahadharisha watendaji katika sekta ya madini ambao watabainika kusababisha migogoro kuwa atawaondoa.

“Migogoro inayosababishwa na watu wangu hasa RMO’s (maofisa madini wakazi ngazi ya mkoa) nataka niwaonye mimi sitawahamisha, nitawaondoa. RMO yeyote ambaye atakuwa chanzo cha migogoro nitawaondoa, tunataka wachimbaji wanufaike na madini.

“Kama mlifikiri kuondoka kwa mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu, Doto Biteko, kwenye sekta ya madini ndio wakati wa kuanza kutorosha madini, ndugu zangu mmepotea, nataka niwaambie sitamuonea mtu aibu, tutashughulika na kila mmoja ambaye anaikosesha mapato nchi yetu…nataka niwaambie ukweli hatutacheka na mtu yeyote kwenye eneo hili,” amesema Mavunde.

Waziri huyo ameahidi kufanya kazi kwa uaminifu na uadilifu ili kukuza sekta ya madini ambayo ina mchango mkubwa katika uchumi wa taifa.

“Namshukuru mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa heshima kubwa aliyonipa ya kuongoza Wizara ya Madini, nataka nimuhakikishie kwamba nitafanya kazi kwa uaminifu na uadilifu mkubwa.

“Nakushukuru mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Madini uliyepita (Dk. Biteko) kwa msingi mzuri uliouweka na kuifanya kazi yangu iwe rahisi, sekta ya madini itakukumbuka daima kwa kazi nzuri na kubwa uliyoifanya,” amesema Mavunde.

Amesema Dk. Biteko ameijengea heshima sekta hiyo, uaminifu na kuifanya kuwa kati ya sekta kiongozi katika kuchangia uchumi wa taifa.

WACHIMBAJI WAKO KWENYE MIKONO SALAMA

Dk. Biteko amewahakikishia wachimbaji kuwa wako kwenye mikono salama kwa kuwa Mavunde ni mchapakazi na kuwataka wamuunge mkono.

“Mavunde nimemfahamu muda mrefu toka tukiwa Umoja wa Vijana, nimemfahamu kama mtu anayejua kusikiliza, hawezi kucheka na upuuzi, anajua kazi aliyopewa inapimika na mwisho wa siku atadaiwa matokeo, ni mtu ambaye anatamani watu watambue yupo inapobidi kutambulika.

“Niwahakikishie wachimbaji wa Tanzania mko kwenye mikono salama, mmepata kijana anayejua kazi, naomba mumtumie, muungeni mkono, vile mlivyofanya kwangu fanyeni zaidi kwake. Pale nilipowakimbiza atawakimbia zaidi kwa haki, anakuja na nguvu mpya ya kusongesha sekta ya madini,” amesema Dk. Biteko.









Powered by Blogger.