DK. BITEKO AITAKA TRA KUWAELIMISHA WACHIMBAJI KODI YA ASILIMIA 2

Naibu Waziri Mkuu, Dk. Doto Biteko, akizungumza wakati wa ufunguzi wa Maonyesho ya Sita ya Kimataifa ya Teknolojia ya Madini katika viwanja vya EPZA mkoani Geita.

Na Nora Damian, Geita
 
Naibu Waziri Mkuu, Dk. Doto Biteko ameitaka Mamalaka ya Mapato Tanzania (TRA) kutoa elimu kwa wachimbaji wadogo kabla ya kuanza kutekeleza agizo la kulipa asilimia mbili wanapouza madini.
 
Akizungumza leo Septemba 23,2023 wakati wa ufunguzi wa Maonyesho ya Sita ya Kimataifa ya Teknolojia ya Madini katika viwanja vya EPZA mkoani Geita, amesema serikali itaendelea kuweka mikakati ya kuendeleza sekta ya madini kwa kuzingatia maendeleo ya mchimbaji mdogo, wa kati na mkubwa.
 
“Nendeni mkawape elimu juu ya hiyo asilimia mbili wailipe wakiwa wanafurahi, kwa sababu tunaitaja kwenye sheria na hata wachimbaji wadogo waliipendekeza wenyewe kwenye majadiliano tuliyokuwa tunayafanya,” amesema Dk. Biteko ambaye pia ni Waziri wa Nishati.

Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, akizungumza wakati wa ufunguzi wa Maonyesho ya Sita ya Kimataifa ya Teknolojia ya Madini katika viwanja vya EPZA mkoani Geita.
 
Aidha amesema uchenjuaji wa madini unaundiwa kanuni mpya na kusisitiza zikamilishwe haraka ili wachenjuaji waweze kutambulika.
 
Dk. Biteko pia ameitaka Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kununua dhahabu kwa bei ya soko na kuwafikia wachimbaji wadogo kokote waliko.
 
“Wachimbaji wadogo hawahitaji maneno, wanahitaji fedha, wafuateni waliko wapeni elimu watawaletea kila gramu wanayoichimba…mkitumia mabavu na sheria hazitawasaidia, wafanyeni rafiki,” amesema.
 
Kuhusu changamoto ya umeme amesema “Mtupe muda, tunakamilisha taratibu Tanesco watakuja na mipango tuliyonayo. Tutahakikisha kero ya umeme tunaipunguza kwa kiasi kikubwa.

Naibu Waziri Mkuu, Dk. Doto Biteko, akipokea tuzo kutoka kwa wachimbaji wa madini kutambua mchango wake katika kukuza sekta hiyo.

Naye Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, amewatahadharisha watendaji katika sekta ya madini ambao watabainika kusababisha migogoro kuwa atawaondoa.

“Mtendaji ambaye atakuwa chanzo cha migogoro mimi sitawahamisha, nitawaondoa. Tunataka wachimbaji wanufaike na madini.
 
“Na kama mlifikiri kuondoka kwa Doto ndio wakati wa kuanza kutorosha madini nataka niwaambie mmepotea…hatutacheka na mtu yeyote kwenye eneo hili,” amesema Mavunde.
 
Waziri huyo ameahidi kufanya kazi kwa uaminifu na uadilifu ili kukuza sekta ya madini ambayo ina mchango mkubwa katika uchumi wa taifa.

Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji, John Bina, akizungumza wakati wa ufunguzi wa Maonyesho ya Sita ya Kimataifa ya Teknolojia ya Madini katika viwanja vya EPZA mkoani Geita.

Kwa upande wake Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji (FEMATA), John Bina, ameiomba Serikali kuwapunguzia kodi kwa madini yanayotoka nje ili yaingie nchini badala ya kupita nchi nyingine.
 
Aidha amesema wanatarajia kuanzisha benki yao ili kuwa na uhakika wa kupata mitaji ya kuendeleza shuguli za uchimbaji.
 
Awali Mkuu wa Mkoa wa Geita, Matrine Shigela, amesema sekta ya madini mkoani humo imepiga hatua ambapo wamewezesha kugawa leseni 1,118 kwa wachimbaji madini walioko Mbogwe na kwa Geita 1,231.
 
Amesema wiki ijayo wanawake 300 wachimbaji madini wa Mkoa wa Geita watakabidhiwa leseni.











Powered by Blogger.