MAVUNDE ATAKA WAWEKEZAJI MADINI KUAJIRI WATU WENYE ULEMAVU
Na Nora Damian, Geita
Waziri wa Madini, Anthony Mavunde amewataka wawekezaji katika sekta ya madini kutekeleza takwa la kisheria la kuwaajiri watu wenye ulemavu ili wanufaike na rasilimali hiyo.
Sheria ya Watu Wenye Ulemavu Namba 9 ya mwaka 2010 inaelekeza mwajiri anayeajiri wafanyakazi zaidi ya 20 katika taasisi za umma au binafsi asilimia tatu wanapaswa wawe watu wenye ulemavu lakini kumekuwa na utekelezaji usioridhisha wa sheria hiyo.
Ameyasema hayo leo Septemba 28,2023 wakati wa kongamano la wadau wa sekta ya madini baada ya Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Foundation for Disabilities Hope (FDH), Maiko Salali, kueleza changamoto katika utekelezaji wa sheria hiyo.
Kongamano hilo lililoshirikisha wadau wa sekta ya madini katika Maonesho ya Sita ya Kimataifa ya Teknolojia ya Madini lililenga kujadili fursa za uwekezaji kupitia Sheria ya Uwezeshaji Wazawa (Local Content).
“Tunahitaji kuwaona Watanzania wengi zaidi wakishiriki katika mnyororo mzima wa kutoa huduma na kuzalisha bidhaa katika migodi yenu.
“Watu wenye ulemavu wana haki sawa ya kushiriki moja kwa moja katika uchumi wa madini, muhakikishe kwamba ushiriki wao unakuwa wa asilimia 100,” amesema Mavunde.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Foundation for Disabilities Hope (FDH), Maiko Salali, akizungumza wakati wa kongamano la wadau wa sekta ya madini kujadili fursa za uwekezaji kupitia Sheria ya Uwezeshaji Wazawa lililofanyika mkoani Geita.Kwa mujibu wa Salali, watu wenye ulemavu wanapoomba nafasi za kazi wamekuwa wakikumbana na changamoto mbalimbali ikiwemo kukosa wakalimani wakati wa usaili.
“Kumekuwa na changamoto mbalimbali kwa watu wenye ulemavu wanapoomba nafasi za kazi ambazo mnaweka kwenye tovuti zenu, kuna watu wenye ulemavu hawaoni, wengine hawasikii. Wanapokuja kwenye usaili mnawatoa nje kwa sababu hamjaweka wakalimani wa lugha ya alama.
“Ni kwa namna gani mmejipanga kuweka mazingira rafiki kwa watu wenye ulemavu pindi mnapotangaza fursa zenu?” amehoji Salali.
Amesema Shirika la Madini la Taifa (Stamico) limekuwa msaada mkubwa kwa watu wenye ulemavu na kushauri kampuni mbalimbali kwenda kujifunza namna linavyowawezesha kiuchumi watu wenye ulemavu.
Mkurugenzi Mtendaji wa Stamico, Dk. Venance Mwasse, ametoa mfano wa kikundi cha viziwi ambacho walikiwezesha kwa kukipatia elimu na mpaka sasa kinajishughulisha na uchimbaji madini.
“Makundi ambayo yanasemekana hayawezi yanaweza, mimi nimejaribu wanaweza, tuna kikundi ambacho tumekilea cha viziwi, tumeanza kuanzia elimu mpaka sasa hivi wanachimba vizuri.
“Ningekuwa mwenyekiti wa kikao hiki hili lingekuwa azimio la leo, tushirikiane kwa kuyaangalia makundi maalumu,” amesema Dk. Mwasse.

