MANUFAA UWEZESHAJI WAZAWA YATAJWA, PROFESA KIKULA AELEZA WALIVYOTUKANWA
Na Nora Damian, Geita
Miaka mitano baada ya kuanza kutekelezwa kwa Sheria ya Uwezeshaji Wazawa (Local Content) mafanikio yameanza kuonekana huku Tume ya Madini ikieleza vikwazo ilivyopitia.
Sheria hiyo ya mwaka 2018 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2019 inalenga kutoa fursa kwa Watanzania kushiriki kikamilifu katika uchumi wa madini.
Mafanikio hayo yameelezwa leo Septemba 28,2023 wakati wa kongamano la wadau wa sekta ya madini kujadili fursa za uwekezaji kupitia sheria hiyo lililofanyika katika Maonesho ya Sita ya Kimataifa ya Teknolojia ya Madini yanayofanyika viwanja vya EPZA Bombambili mkoani Geita.
Kamishna wa Local Content, Janeth Lukeshingo, amesema ajira zimeongezeka, manunuzi ya bidhaa na huduma kwa Watanzania, ushirikishwaji na uwaulishaji wa teknolojia na utafiti, maendeleo na kuongezeka kwa uelewa kuhusu ushirikishwaji wa Watanzania katika seta ya madini.
Wawekezaji
Mratibu wa Local Content katika Kampuni ya Geita Gold Mining Limited, Riwald Tenga, amesema wanatekeleza sheria hiyo kwa asilimia 90.
“Tunafuata masharti yote katika manunuzi na katika utoaji ajira, yote tunayofanya kwenye Local Content tuko kati ya asilimia 60 mpaka 90,” amesema Tenga.
Kampuni inayojihusisha na usafirishaji na usambazaji wa bidhaa na mizigo ya Blue Coast Investment imesema imenufaika kwa kufanya kazi na GGML.
Masumbuko Thobias wa Kampuni ya Busolwa amesema kwa siku wanazalisha tani 1,200 hivyo wanahitaji bidhaa na huduma mbalimbali kutoka katika taasisi na watu binafsi na kuwakaribisha watu kuchangamkia fursa hizo.
Washiriki wakifuatilia kongamano la kujadili fursa za uwekezaji kupitia Sheria ya Local Content lililofanyika mkoani Geita. Kushoto ni Mbunge wa Geita Mjini, Costantine Kanyasu.Dhana ya Local Content
Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula, amesema dhana ya Local Content ilikuwa mpya wakati tume hiyo inaanza lakini hivi sasa imeanza kueleweka.
“Watu waliturushia matusi kuhusu Local Content lakini tukajikaza, siwezi kusema ni kina nani walikuwa wanatutukana lakini tulipata matusi ambayo si ya kawaida na ambao walifanya hivyo mmoja alikuwa mwanasheria na yupo mpaka leo.
“Tulitukanwa kwa sababu kuna watu walikuwa hawajaielewa lakini tumefikia mahali ambapo panastahili,” amesema Profesa Kikula.
Mbunge wa Geita Mjini, Costantine Kanyasu, amesema baada ya marekebisho ya sheria hiyo wameanza kuona manufaa na kuipongeza Serikali kwa kuisimamia.
“Baada ya kuanza kutekelezwa kwa Local Content hasira ya wananchi imepungua, wengi wanashiriki, wanajishughulisha na uuzaji na usambazaji wa bidhaa wenye migodi mbalimbali,” amesema Kanyasu.
Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigela, ameshauri uzoefu uliopatikana katika sekta ya madini uendelezwe katika sekta nyingine.
“Tukifanya hivi itatusaidia kuendeleza ujuzi na uelewa kwa Watanzania ili wengi zaidi washiriki katika sekta nyingine,” amesema Shigela.
Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika kongamano hilo amesema ndani ya muda mfupi ushiriki wa Watanzania umeongezeka katika sekta ya madini.
“Tumejifunza kuna mambo lazima twende tukayafanyie kazi kwa haraka, Local Content inagusa maisha na uchumi wa Watanzania.
“Profesa Kikula moja ya alama ambayo utaiacha tena katika mioyo ya Watanzania na hasa wadau wa sekta ya madini ni namna ulivyosimamia Sheria ya Local Content…matokeo tumeanza kuyaona.
“Mwenyekiti wa Kamati ya Local Content amefanya mapinduzi makubwa ndani ya muda mfupi, amekuwa kwenye sekta hii kwa zaidi ya miaka 18, hakuna jambo ambalo unaweza kumuongopea,” amesema Mavunde.

