BLUE COAST YAELEZA ILIVYONUFAIKA NA LOCAL CONTENT IKIITAJA GGML

Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, akizungumza baada ya kutembelea Kampuni ya Blue Coast iliyopo mkoani Geita.

Na Nora Damian, Geita

Kampuni inayojihusisha na usafirishaji na usambazaji wa bidhaa na mizigo ya Blue Coast Investment imesema imenufaika na kuwepo kwa Sheria ya Ushirikishwaji Wazawa (Local Content) kwa kufanya kazi na Kampuni ya GGML.

Kampuni hiyo imesema GGML imekuwa chachu ya wao kufikia viwango vya ubora kwa kuwa imewapatia elimu kwa lengo la kuendelea kufanya biashara endelevu.

Akizungumza Septemba 27,2023 baada ya Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, kutembelea kampuni hiyo mkoani Geita, Mkurugenzi Mtendaji wa Blue Coast, Ndahilo Athanas, amesema wameanza kufanya biashara na GGML tangu mwaka 2021.

“Tunaishukuru Serikali kwa kuona umuhimu wa sheria hii na kuipitisha, lakini tunamshukuru zaidi Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kusimamia utekelezaji wa sheria hii.

“GGML wana mchango mkubwa wa kutufikisha hapa tulipo, wamekuwa chachu ya sisi kufikia viwango vya ubora. Wametupatia elimu ya kutosha juu ya umuhimu wa ubora na namna ya kuendelea kufanya biashara endelevu,” amesema Athanas.

Waziri wa Madini, Anthony Mavunde (Kushoto), akizungumza na viongozi wa Kampuni ya Blue Coast. Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Ndahilo Athanas na Katikati ni Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigela.

Amesema wanaendesha shughuli zao kupitia viwango vya kitaifa na kimataifa ambapo wana cheti cha usalama kazini, cheti cha ubora wa kazi na sasa wanaendelea na usajili wa ubora katika usimamizi wa mazingira.

Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, kampuni hiyo imeajiri zaidi ya wafanyakazi 360 kwenye ajira rasmi na zisizo rasmi kwa wakazi wa Geita na maeneo mengine yanayozunguka mkoa huo na kufanya idadi kufikia 580 kutoka 220 wa mwaka 2021.

Aidha amesema wamejikita kutoa elimu kazini ili kuwajengea uwezo vijana kabla ya kuwapa ajira rasmi hasa wahitimu wa vyuo vikuu.

“Mpaka sasa vijana 46 wameajiriwa kupitia utaratibu huu katika nyanja mbalimbali kama uhasibu, maofisa ugavi, mafundi magari, maofisa uendeshaji na nyingine,” amesema.

Mkurugenzi huyo amesema pia wamepata tuzo ya mlipakodi bora kwa Mkoa wa Geita na kwamba kupitia fursa ya Local Content kampuni hiyo imekua na sasa imehamishiwa kwenye kundi la walipakodi wakubwa.

Kuhusu kusaidia jamii amesema wametoa Sh milioni 150 kwa ajili ya uboreshaji wa elimu katika shule za msingi.

Waziri Mavunde ameipongeza kampuni hiyo na kuzitaka kampuni zingine kuchangamkia fursa katika sekta ya madini ili kutoa ushindani kwa wawekezaji wa ndani na nje.

“Nawaomba Watanzania wajitokeze pindi nafasi mbalimbali zinapotangazwa kwa sababu hiki ndicho kitakuwa kipimo chetu cha kutoa huduma na kuzalisha bidhaa kwa viwango vya kimataifa,” amesema Mavunde.

Mwenyekiti wa Blue Coast, Athanas Inyasi, ameishukuru Serikali kwa kutunga sheria hiyo ambayo imewawezesha kupata fursa ya kufanya biashara na migodi mikubwa.





Powered by Blogger.