GCLA YASISITIZA WANAOJIHUSISHA NA KEMIKALI KUJISAJILI

Mkaguzi wa Kemikali kutoka katika Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) Kanda ya Ziwa, Zachariah Deus, akizungumza wakati wa kongamano la wadau wa sekta ya madini lililofanyika katika Maonyesho ya Sita ya Teknolojia ya Madini mkoani Geita.

Na Nora Damian, Geita

Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) imewataka wadau wote wanaojihusisha na shughuli za kemikali wakiwemo wachimbaji wa madini kujisajili.

Sheria ya Usimamizi na Udhibiti wa Kemikali za Viwandani na Majumbani Namba 3 ya mwaka 2003 inaelekeza hivyo ili kuhakikisha kunakuwa na matumizi sahihi ya kemikali.  

Akizungumza Septemba 22,2023 Mkaguzi wa Kemikali kutoka katika mamlaka hiyo Kanda ya Ziwa, Zachariah Deus, amesema wamekuwa wakitoa elimu ya matumizi sahihi ya kemikali na kuwasajili wote wanaojishughulisha nazo. 

Mtekinolojia Mkuu kutoka Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA), Christer Mwageni, akimweleza Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe, shughuli za mamlaka hiyo baada ya kutembelea Maonyesho ya Sita ya Teknolojia ya Madini mkoani Geita.

Mkaguzi huyo alikuwa akizungumza wakati wa kongamano la wadau wa sekta ya madini lililofanyika katika Maonyesho ya Sita ya Teknolojia ya Madini yanayofanyika viwanja vya EPZA mkoani Geita.

“Kemikali zisipotumika kwa namna ambayo ni sahihi zimebeba athari kubwa, kuna kuchafua mazingira kuna kuhatarisha afya ndiyo maana tunalo jukumu kubwa la kusimamia sheria. 

“Kifungu cha 22 kifungu kidogo cha kwanza kinatamka wazi kwamba kutakuwepo na vyeti vya usajili; cheti cha usajili cha awali kitadumu kwa miaka miwili na cheti kamili kitadumu kwa miaka mitano,” amesema Deus.

Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe, 
akizungumza wakati wa kongamano la wadau wa sekta ya madini lililofanyika katika Maonyesho ya Sita ya Teknolojia ya Madini mkoani Geita.

Amesema pia kuna miongozo ya uagizaji na utumiaji wa kemikali mbalimbali ikiwemo uingiza na utumiaji wa zebaki.

Kemikali ya zebaki au mekyuri imekuwa ikitumiwa na wachimbaji hasa wakati wa kuamatisha dhahabu na inatajwa kuwa na madhara ya kiafya kwa binadamu na kuharibu mazingira.

Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika kongamano hilo amesema mazingira bora ya ufanyaji biashara Tanzania yanawezekana na kuwataka wachimbaji kujitahidi kujua na kuelewa taratibu za namna ya kupata leseni na huduma mbalimbali zinazotolewa na taasisi za umma.

“Sisi kama Serikali kupitia taasisi hizi tuna kazi ya ziada ya kuhakikisha tunaendelea kutoa elimu ya jinsi ambavyo tunatakiwa kuwahudumia Watanzania katika seta zote hasa sekta ya madini.

“Majukumu yawe ni kuwasaidia, suala la kwamba amekosea tusingependa kuona wanakosea, tuwaambie taratibu na kanuni za ufanyaji biashara mbalimbali. Tuhakikishe tunaendelea kuwapa elimu wajue taratibu, kanuni na sheria ili tusifike sehemu ya kuwapa adhabu.

“Changamoto kubwa ni elimu, Watanzania wengi sasa wameamka, wachimbaji wadogo mchango wao ni mkubwa kwahiyo ni vema tuhakikishe tunawasaidia wawe wa kati na baadaye wawe wakubwa, tusipowalea tutaendelea kuona makampuni makubwa ya nje,” amesema Kigahe.



Powered by Blogger.