CRDB YAWATOA HOFU WACHIMBAJI WANAWAKE UPATIKANAJI MITAJI

Meneja Biashara wa Benki ya Crdb Kanda ya Magharibi, Anselem Mwenda, akizungumza wakati wa kongamano la miaka 25 ya Chama cha Wanawake Wachimbaji Tanzania (Tawoma) lililofanyika katika Maonesho ya Sita ya Kimataifa ya viwanja vya EPZA Bombambili, mkoani Geita.

Na Nora Damian, Geita

Benki ya Crdb imewahakikishia wanawake wachimbaji kuwa itaendelea kuwawezesha kwa kuwapatia mikopo waweze kunufaika na rasilimali za madini nchini.

Akizungumza Septemba 29,2023 Meneja Biashara wa Benki ya Crdb Kanda ya Magharibi, Anselem Mwenda, amesema wako kwenye mazungumzo na mifuko ya dhamana ili kurahisisha upatikanaji wa mikopo kwa wanawake wachimbaji.

Mwenda alikuwa akizungumza wakati wa kongamano la miaka 25 ya Chama cha Wanawake Wachimbaji Tanzania (Tawoma) lililofanyika katika Maonesho ya Sita ya Kimataifa ya viwanja vya EPZA Bombambili, mkoani Geita.

“Tunajisikia furaha kuwa sehemu ya kufanikisha mafanikio ya kinamama katika nchi hii, ndio maana katika suala lolote linalohusu kinamama huwezi kutukosa Crdb.

“Iko mifuko ya dhamana kama benki tunashirikiana na mifuko mingi ya dhamana, kazi ya mifuko ni kuhakikisha kama mteja ambaye hana dhamana ya kutosha lakini anafanya shughuli zake vizuri na ana uhitaji wa mtaji, benki inampa mtaji kwa kuchukua dhamana ya ule mfuko asilimia fulani.

“Kwahiyo tuko kwenye mazungumzo na mifuko ya dhamana, nataka niwatoe hofu kabisa kwamba tutakopesha na mtaweza kupata mitaji hata kama suala la dhamana halijakaa vizuri.

“Kuweni na amani kikubwa muonyeshe nguvu ya kutosha, muonyeshe jitihada na muwe tayari kuingia katika hayo majukumu,” amesema Mwenda.

Amesema pia tayari wamebuni bidhaa maalumu kusaidia wachimbaji wadogo nchini wakiwemo wanawake wanaojihusisha na shughuli hizo ambayo imeanza kutekelezwa katika maeneo ya Mbogwe, Kakola na Nyang’wale mkoani Geita.

“Tayari tumeanza kukopesha wachimbaji wadogo katika maeneo yenye uhitaji mkubwa ikiwemo ulipaji wa vibarua, ununuzi wa kemikali na mahitaji mengine.

“Ni bidhaa inayofanya vizuri, katika yale maeneo hatujakutana na changamoto yoyote, tutaongeza maeneo ili kuwafikia kinamama wengi zaidi,” amesema Mwenda.

Amesema pia wako kwenye hatua za mwisho za kuandaa andiko la bidhaa maalumu kwa kinamama hasa wachimbaji.

Meneja huyo amewahamasisha kinamama walio kwenye vikundi kuchangamkia fursa za benki hiyo zinazotolewa kupitia vikundi.







Powered by Blogger.