CRDB YANADI BONDI YA KIJANI KWA WADAU WA MADINI
Meneja wa Crdb Kanda ya Magharibi, Jumanne Wagana, akimkabidhi zawadi Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Hemed Suleiman (kulia), alipotembelea banda la benki hiyo kwenye Maonesho ya Sita ya Teknolojia ya Madini yaliyofanyika viwanja vya EPZA Bombambili mkoani Geita.
Na Nora Damian, Geita
Benki ya Crdb imewahamasisha wadau wa sekta ya madini kuchangamkia fursa ya hatifungani ya kijani (Kijani Bond) ambayo wanaweza kupata faida ya riba ya asilimia 10.2 kwa mwaka.
Kupitia hatifungani hiyo ilizinduliwa hivi karibuni benki hiyo inatarajia kukusanya Sh bilioni 40 kutoka kwenye uwekezaji huo katika awamu ya kwanza.
Leo Septemba 30,2023 Meneja wa Crdb Kanda ya Magharibi, Jumanne Wagana, ametumia Maonesho ya Sita ya Teknolojia ya Madini yaliyofanyika viwanja vya EPZA Bombambili mkoani Geita kunadi hatifungani hiyo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Hemed Suleiman (kulia), akimsikiliza Meneja wa Crdb Kanda ya Magharibi, Jumanne Wagana, alipotembelea banda la benki hiyo kwenye Maonesho ya Sita ya Teknolojia ya Madini yaliyofanyika viwanja vya EPZA Bombambili mkoani Geita.
Wagana alikuwa akizungumza baada ya Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Hemed Suleiman, kutembelea banda la benki hiyo.
“Tunatoa huduma za kibenki ambapo wateja wanaweza kufungua akaunti, tunawapa elimu kuhusu huduma mbalimbali kama tuliyonayo sasa ambayo inaitwa Bondi ya Kijani. Wadau wa madini wanaweza kuwekeza na kuvuna faida ya asilimia 10.2,” amesema Wagana.
Amesema benki hiyo inashirikiana na sekta ya madini ambapo wamekuwa wakifanya uwezeshaji wa mitambo, wanunuzi, wachimbaji na wachenjuaji wa madini.
Amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi kwa ushirikiano wanaoipatia benki hiyo hasa katika miradi ya kimkakati ya Serikali kama vile ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), bomba la mafuta na mingine.
Meneja huyo amesema kwa upande wa Zanzibar benki hiyo ilitenga Sh bilioni 300 kusapoti Sera ya Uchumi wa Buluu na kuwanakopesha wajasiriamali bila riba.
Mbali ya kushiriki maonesho hayo benki hiyo pia ni moja ya wadhamini wa maonesho hayo.
Mbali ya kushiriki maonesho hayo benki hiyo pia ni moja ya wadhamini wa maonesho hayo.

