BRELA YAWAFUNDA WACHIMBAJI FAIDA LESENI ZA BIASHARA
Mkuu wa Idara ya Miliki Ubunifu Brela, Loy Mhando (kushoto), akimkabidhi cheti mkazi wa Geita baada ya kusajili jina la biashara kwenye Maonesho ya Sita ya Teknolojia ya Madini yanayofanyika viwanja vya EPZA mkoani Geita.
Na Nora Damian, Geita
Wakala ya Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) umewataka wachimbaji na wafanyabiashara wa madini kusajili na kurasimisha majina, alama za biashara na huduma ili kufanya shughuli zao kihalali.
Brela inatoa leseni za kundi A ambazo ni za biashara za kitaifa na kimataifa ikiwemo za viwanda.
Akizungumza Septemba 22, 2023 wakati wa mafunzo maalumu kwa wachimbaji na wafanyabiashara wa madini, Ofisa Leseni kutoka Brela, Jubilate Muro, amesema leseni ya biashara ni takwa la kisheria na hakuna mtu yeyote anayeruhusiwa kufanya biashara bila kuwa na leseni.
Ofisa huyo alikuwa akizungumza wakati wa Siku ya watoa huduma na leseni za uchimbaji madini na uwezeshaji mitaji kwa washiriki wa Maonyesho ya Sita ya Teknolojia ya Madini yanayofanyika viwanja vya EPZA mkoani Geita.
Ofisa Leseni kutoka Brela, Jubilate Muro, akizungumza wakati wa Siku ya watoa huduma na leseni za uchimbaji madini na uwezeshaji mitaji kwa washiriki wa Maonyesho ya Sita ya Teknolojia ya Madini yanayofanyika viwanja vya EPZA mkoani Geita.
“Ni muhimu kuwa na leseni za biashara kwa sababu zinaiwezesha Serikali kupata takwimu sahihi zinazohusiana na biashara hapa nchini na kumwezesha mfanyabiashara kutambulika na taasisi za kifedha ili aweze kupata mikopo mfano kwenye mabenki,” amesema Muro.
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika siku hiyo amesema mazingira bora ya ufanyaji biashara Tanzania yanawezekana na kuwataka wachimbaji kujitahidi kuelewa taratibu za namna ya kupata leseni na huduma mbalimbali zinazotolewa na taasisi za umma.
“Sisi kama Serikali kupitia taasisi hizi tuna kazi ya ziada ya kuhakikisha tunaendelea kutoa elimu ya jinsi ambavyo tunatakiwa kuwahudumia Watanzania katika seta zote hasa sekta ya madini.
“Majukumu yawe ni kuwasaidia, suala la kwamba amekosea tusingependa kuona wanakosea, tuwaambie taratibu na kanuni za ufanyaji biashara mbalimbali. Tuhakikishe tunaendelea kuwapa elimu wajue taratibu, kanuni na sheria ili tusifike sehemu ya kuwapa adhabu.
“Changamoto kubwa ni elimu, Watanzania wengi sasa wameamka, wachimbaji wadogo mchango wao ni mkubwa kwahiyo ni vema tuhakikishe tunawasaidia wawe wa kati na baadaye wawe wakubwa, tusipowalea tutaendelea kuona makampuni makubwa ya nje,” amesema Kigahe.

Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe, akizungumza wakati wa Siku ya watoa huduma na leseni za uchimbaji madini na uwezeshaji mitaji kwa washiriki wa Maonyesho ya Sita ya Teknolojia ya Madini yanayofanyika viwanja vya EPZA mkoani Geita.
Mkuu wa Idara ya Miliki Ubunifu Brela, Loy Mhando, amesema watazingatia maagizo yote yaliyotolewa na Naibu Waziri Kigahe na kuahidi kuwahudumia wafanyabiashara kwa ufanisi zaidi.
"Tumepokea maelekezo ya Naibu Waziri na tutahakikisha tunawafikia wafanyabiashara popote walipo ili waweze kupata huduma kwa wakati," amesema Mhando.
Katika maonesho hayo Brela inatoa huduma za papo kwa papo ambazo zinahusisha usajili wa majina ya biashara, kampuni, utoaji wa leseni za biashara kundi A na usajili wa viwanda vidogo.
“Kutokana na elimu tunayoendelea kuitoa watu wengi wamehamasika wanakuja tunawapa usaidizi wa kuwasajili na kuwarasimishia biashara wanaondoka na vyeti vyao,” amesema Mhando.