WENZA WANAOTAKA KUTOA FIGO LAZIMA WATHIBISHWE KISHERIA


Mratibu wa Huduma za Upandikizaji Figo kutoka Hospitali ya Benjamin Mkapa, Awadhi Mohamed (kulia), akimsikiliza mwananchi aliyetembelea banda la hospitali hiyo kwenye Maonesho ya Nanenane Kitaifa viwanja vya John Mwakangale, jijini Mbeya.

Na Nora Damian, Mbeya

Wagonjwa ambao figo zao hazifanyi kazi na kutakiwa kupandikizwa nyingine kutoka kwa binadamu aliye hai kama vile wenza wao watatakiwa kuwa na uthibitisho wa kisheria kukwepa watu kuingia katika biashara ya kuuza viungo.

Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) tangu mwaka 2018 mpaka sasa imepandikiza figo wagonjwa 35 na kati yao wanne wamechangiwa na wenza wao.

Akizungumza Agosti 5, 2023 na waandishi wa habari Mratibu wa Huduma za Upandikizaji Figo kutoka Hospitali ya Benjamin Mkapa, Awadhi Mohamed, amesema kati ya wagonjwa 35 watatu ni kutoka nje ya nchi.

Alikuwa akizungumza kwenye Maonesho ya Nanenane Kitaifa viwanja vya John Mwakangale, jijini Mbeya ambapo hospitali hiyo inatoa huduma za dharura, macho, pua, masikio na koo pamoja na kuelimisha umma kuhusu matibabu ya ubingwa bobezi.

“Mtu ambaye anasema ana mwenza ni lazima awe ni mwenza kweli, sio ndoa iliyofungwa jana halafu leo akasema huyu ni mke wangu au ni mume wangu nataka nichangie figo.

“Ni lazima timu ijiridhishe kwa kufanya ufuatiliaji kuona kweli uhusiano uko sahihi…pengine inaweza kuwa biashara imefanyika,” amesema Mohamed.


Kwa mujibu wa mratibu huyo, kwa vigezo ambavyo dunia imeweka mwenza anaingia katika kundi la pili iwapo atakosekana mchangiaji kwenye kundi la kwanza lenye uhusiano wa moja kwa moja.

“Kundi la kwanza lenye uhusiano wa moja kwa moja tunaweza tusimpate mtu kutokana na vigezo vya kiafya, pengine watu waliopo wana shida nyingine za kiafya au makundi yao ya damu yanatofautiana au wana magonjwa ambayo hayaruhusu wachangie, au pengine umri umezidi au uko chini ya ule unaotakiwa.

“Kwenye kundi la pili wako wenza, anaweza kuwa mke au mume lakini lazima akubali kwa hiyari yake, akishakubali tunafanya uthibitisho kama kweli ni wenza kisheria kisha tunafanya vipimo kwa kuzingatia vigezo vyote,” amesema.

Amesema tahadhari hiyo ni muhimu kwani njama zinaweza kufanyika kwa watu kuuzwa, kutekwa au viungo kuvunwa bila hiyari yao na kuuzwa.

“Dunia iliweka tahadhari hiyo ili kama hakutakuwa na sheria na utaratibu mzuri uchangiaji ufanyike kwa watu wa karibu kwa maana ya ndugu na watu wenye uhusiano wa karibu,” amesema Mohamed.








Powered by Blogger.