MAFUTA YA PARACHICHI YAWA DILI, LITA MOJA SH 35,000
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe, akiangalia mafuta ya parachichi baada ya kutembelea banda la Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda Tanzania (TIRDO) kwenye Maonesho ya Nanenane Kitaifa viwanja vya John Mwakangale, jijini Mbeya. Kulia ni Mtafiti wa shirika hilo, Paul Kimath.
Na Nora Damian, Mbeya
Ni kicheko kwa wakulima wa parachichi baada ya kubuniwa kwa teknolojia ya kuliongezea thamani zao hilo ya kuzalisha mafuta yanayouzwa kati ya Sh 25,000 hadi 35,000 kwa lita.
Teknolojia hiyo ya mashine ya kuchakata mafuta ya parachichi imebuniwa na Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda Tanzania (TIRDO).
Shirika hilo linatumia Maonesho ya Nananane Kitaifa yanayofanyika viwanja vya John Mwakangale, jijini Mbeya kunadi teknolojia hiyo na kuwaelimisha wakulima kuhusu uchakataji wa mafuta ya parachichi.
Akizungumza Agosti 4, 2023 na waandishi wa habari Mtafiti kutoka TIRDO, Paul Kimath, amesema parachichi ikiongezewa thamani itakuwa na tija kwa wananchi wa Mikoa ya Nyanda za Juu na mingine inayolima zao hilo.
“Mikoa ya Ukanda wa Nyanda za Juu kuanzia Iringa, Njombe, Mbeya na Songwe wanalima sana parachichi lakini masoko yamekuwa yanawapa shida.
"Mahitaji ya mafuta ya parachichi ni makubwa ndiyo maana tumebuni mashine hii na tunawahamasisha wakulima kutumia fursa kwa kuzalisha kwa wingi parachichi,” amesema Kimath.
Kwa mujibu wa mtafiti huyo, mafuta ya parachichi yana matumizi mengi kwani yanaweza kutumika kama chakula na kutengenezea vitu mbalimbali kama vile bidhaa za usafi na urembo.
“Mafuta ya parachichi yana vitamin A kwa wingi na E ambayo ni malighafi muhimu katika bidhaa za urembo na usafi. Wananchi wa mikoa hii (Nyanda za Juu) na mingine inayolima parachichi kama Kilimanjaro waje Tirdo wajifunze jinsi ya kuchakata mafuta ya parachichi,” amesema.
Kwa mujibu wa mtafiti huyo, mafuta ya parachichi yana matumizi mengi kwani yanaweza kutumika kama chakula na kutengenezea vitu mbalimbali kama vile bidhaa za usafi na urembo.
“Mafuta ya parachichi yana vitamin A kwa wingi na E ambayo ni malighafi muhimu katika bidhaa za urembo na usafi. Wananchi wa mikoa hii (Nyanda za Juu) na mingine inayolima parachichi kama Kilimanjaro waje Tirdo wajifunze jinsi ya kuchakata mafuta ya parachichi,” amesema.
Mtafiti kutoka Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda Tanzania (TIRDO), Paul Kimath (kulia), akimuonesha Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe, mashine ya kuchakata mafuta ya parachichi kwenye Maonesho ya Nanenane Kitaifa viwanja vya John Mwakangale, jijini Mbeya.
Akizungumzia soko la mafuta hayo amesema ni kubwa na kwa sasa lita moja inauzwa kati ya Sh 25,000 hadi 35,000.
Aidha amesema wanatafuta wawekezaji kwa ajili ya kuwekeza katika uzalishaji wa mafuta hayo hasa wajasiriamali wadogo ambapo pia wanatembelea vikundi mbalimbali katika halmashauri kuhamasisha waanze uzalishaji.
Mtafiti huyo amesema mashine hiyo thamani yake ni Sh milioni 5.5 ambayo inajumuisha mashine, vifaa pamoja na mafunzo ya uchakataji wa mafuta.
Kwa upande wake Kigahe amelitaka shirika hilo kuhakikisha wanawafikia wananchi ili tafiti zilizofanyika ziwe na manufaa kwa taifa.

