VETA YAJA NA SULUHISHO UTENGENEZAJI CHAKULA CHA MIFUGO
Mkufunzi wa Chuo cha Veta Songea, Sussack Mbulu, akionesha mashine ya kuchakata chakula cha mifugo kwenye Maonesho ya Nanenane Kitaifa viwanja vya John Mwakangale, jijini Mbeya.
Na Nora Damian, Mbeya
Chuo cha Ufundi Stadi Veta Songea kimetengeneza mashine ya kuchakata chakula cha kuku na samaki kilicho kwenye mfumo wa punjepunje.
Mashine hiyo iliyobuniwa na Mkufunzi wa Chuo cha Veta Songea, Sussack Mbulu, ina uwezo wa kuzalisha kilo 100 kwa siku.
Akizungumza Agosti 5, 2023 na waandishi wa habari kwenye Maonesho ya Nanenane Kitaifa viwanja vya John Mwakangale, jijini Mbeya amesema ni rahisi kutumiwa na wafugaji wadogo wadogo kuzalisha chakula badala ya kutegemea mashine kubwa.
“Chakula kinakuwa kwenye mfumo wa punjepunje kwa sababu virutubisho vyote vinajumuishwa kwenye kipande kimoja, kuku au samaki akila kitamfanya awe na afya njema kuliko utaratibu uliokuwa ukitumika siku za nyuma wa kupalaza mahindi na kuweka kwenye mfumo wa chengachenga.
“Ukichanganya dagaa na mahindi kuku anaweza akaamua kula dagaa tu, badala ya kumfuga miezi miwili unakuta unamfuga miezi sita mfugaji atapata hasara.
“Teknolojia hii itapunguza gharama za ununuzi wa chakula na hata kwa wanafunzi wetu wanaweza kujiajiri kwa kutengeneza mashine au kuuza chakula,” amesema Mbulu.
Mfugaji kutoka Wilaya ya Momba mkoani Songwe, Zuberi Paulo (kulia), akiangalia jinsi mashine ya kuchakata chakula cha mifugo inavyofanya kazi kwenye Maonesho ya Nanenane Kitaifa viwanja vya John Mwakangale, jijini Mbeya.Ametoa wito kwa jamii kutembelea vyuo vya Veta ili kujifunza na kupata mashine hizo kisha kujiajiri na kuongeza kipato kwa vijana na wanawake ambao wengi ni wafugaji.
“Kwa wanaofuga samaki hii ni fursa kwa sababu mashine hii inatengeneza chakula ambacho kinaelea,” amesema.
Kwa mujibu wa Mbulu, mashine hiyo inauzwa kwa Sh 300,000 na tayari watu mbalimbali wameomba kutengenezewa.
Mmoja wa wakulima na mfugaji kutoka Wilaya ya Momba mkoani Songwe, Zuberi Paulo, amesema amekuwa akipata changamoto ya magonjwa ya kuku na vyakula hasa upatikanaji wa soya.
“Nimefurahishwa na mashine hii kwanza inaondoa vumbi kwenye chakula cha kuku kwahiyo watakuwa hawapati mafua na gharama za dawa zitapungua.
“Kuna changamoto ya upatikanaji wa vyakula vya kuku na namna ya kuvichanganya, nikiwa na mashine hii itanisaidia kurahisisha zoezi la uchanganyaji na kupata chakula ambacho ni kikavu,” amesema Paulo.

