‘WANANCHI WAELIMISHWE MATUMIZI SALAMA YA MIONZI’

Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo Zanzibar, Shamata Khamis (katikati) akipata maelezo kutoka kwa Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC), Peter Ngamilo, alipotembelea banda la tume kwenye Maonesho ya Nanenane Kitaifa viwanja vya John Mwakangale, jijini Mbeya.


Na Nora Damian, Mbeya

Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC) imeshauriwa kuendelea kuelimisha umma kuhusu matumizi salama ya mionzi kwa maendeleo endelevu ya kijamii na kiuchumi. 

Tume hiyo inafanya kazi ya kudhibiti na kusimamia vifaa vyote vitoavyo mionzi pamoja na kufanya ukaguzi wa vituo zaidi ya 320 vitoavyo huduma ya mionzi nchini ili kujiridhisha usalama wake.

Ushauri huo umetolewa Agosti 6, 2023 na Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo Zanzibar, Shamata Khamis, baada ya kutembelea banda la tume hiyo kwenye Maonesho ya Nanenane Kitaifa viwanja vya John Mwakangale, jijini Mbeya. 

“Imarisheni utaratibu wa ufikashaji taarifa kwa wananchi hasa walioko katika maeneo ya vijijini kuhusu kujilinda na madhara yatokanayo na mionzi,” amesema Khamis.

Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano TAEC, Peter Ngamilo, amesema kama wakibaini kuna mionzi iliyozidi huwa wanapeleka wataalam kuangalia wakibaini tatizo husimamisha huduma.

“Kama tukikuta mashine mbovu tunasimamisha huduma mashine inatengenezwa ikishatengemaa tunaruhusu iendelee kutoa huduma, Tukigundua mtoa huduma amepata kiasi cha mionzi ambacho hapaswi kukipata tunashauri abadilishiwe mazingira ya kufanya kazi kwa sababu tabia ya seli za binadamu ukipata hilo tatizo kuna baadhi ya seli zinakufa,” amesema Ngamilo.


 Akitoa elimu juu ya matumizi salama ya mionzi


Amesema wanatumia fursa za maonesho kutoa elimu kwa wananchi sambamba na vipindi kwenye vyombo vya habari kama redio na televisheni.

“Tunatumia mitandao ya kijamii katika kuhakikisha kwamba tunafikisha elimu kwa wananchi,” amesema. 

Amesema kazi za tume hiyo ni kukagua vituo vyote vyenye vyanzo vya mionzi ili kusimamia utekelezaji wa sheria, kutoa vibali vya uagizaji, umiliki, utumiaji wa vyanzo vya mionzi.

Zingine ni kupima sampuli za vyakula, mbolea, vyakula vya wanyama, tumbaku na mazao yake vinavyoingizwa na kusafirishwa nje ya nchi.

“Tunapima sampuli za mazingira kubaini uchafuzi wa mionzi kwenye mazingira, kupima kiwango cha mionzi kwenye minara ya simu na rada za mawasiliano, kukusanya, kusafirisha na kuhifadhi mabaki ya vyanzo vya mionzi,” amesema Ngamilo.




Powered by Blogger.