REMIGIA MBANGA: TUNAJIVUNIA KUWANYANYUA WANACHAMA KIUCHUMI
Mwenyekiti wa Chama cha Akiba na Mikopo cha Amkeni Saccos, Remigia Mbanga, akizungumza kuhusu mafanikio ya chama hicho wakati wa Maonesho ya Nanenane Kitaifa viwanja vya John Mwakangale, jijini Mbeya.
Na Nora Damian, Mbeya
Chama cha Akiba na Mikopo cha Amkeni Saccos kilichopo mkoani Mbeya kinajivunia kuwanyanyua wanachama wake kiuchumi kwa kuwapatia mikopo mbalimbali.
Chama hicho kilichopo eneo la Ilomba Mbeya Mjini kilianzishwa Januari mwaka 2009 na mpaka sasa kina wanachama 233.
Akizungumza Agosti 6, 2023 katika banda lao lililopo Kijiji cha Ushirika kwenye Maonesho ya Nanenane Kitaifa viwanja vya John Mwakangale, jijini Mbeya Mwenyekiti wa chama hicho, Remigia Mbanga, amesema wanatoa mikopo kwa wanachama kwa lengo la kuwakomboa kiuchumi.
Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo, mikopo hiyo ni pamoja na fedha taslimu, bajaji na pikipiki na mingine.
“Wanachama wengi wamebadilisha maisha yao baada ya kujiunga na Saccos yetu, wamepata mafanikio mbalimbali wapo waliojenga nyumba, kusomesha watoto na kuanzisha biashara zenye tija.
"Kwenye maonesho haya tunaonesha kazi mbalimbali tunazozifanya na kuwahamasisha wananchi kujiunga na chama kwa sababu ni mkombozi kiuchumi," amesema Mbanga.
Chama hicho kimetoa wito kwa wakazi wa maeneo mbalimbali ya Mbeya kujiunga ili waweze kupata fursa zitakazowakomboa kiuchumi.
