BRELA KUHUISHA MIFUMO UTOAJI LESENI ZA BIASHARA


Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe, akizungumza baada ya kutembelea banda la Wakala ya Usajili wa Biashara na Leseni kwenye Maonesho ya Nanenane Kitaifa viwanja vya John Mwakangale, jijini Mbeya. Katikati ni Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano BRELA, Roida Andusamile.

Na Nora Damian, Mbeya

Wakala ya Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) una mpango wa kuhuisha mifumo yake na mingine ili kurahisisha utoaji huduma kwa wananchi.

Kwa sasa Brela inao mfumo wa usajili kwa njia ya mtandao (ORS) ambao unawezesha kupata cheti cha usajili wa kiwanda kidogo au leseni ya kiwanda, alama za biashara na huduma.

Hayo yamesemwa leo Agosti 5, 2023 na Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano BRELA, Roida Andusamile, kwenye Maonesho ya Nanenane Kitaifa viwanja vya John Mwakangale, jijini Mbeya.

Roida alikuwa akizungumza baada ya Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe, kutembelea banda la wakala huo na kutaka kujua namna inavyoshirikiana na taasisi zingine katika utoaji huduma hasa baada ya kuwapo kwa mabadiliko ya mifumo mbalimbali ukiwemo mfumo mpya wa Tausi.

“Tuna mfumo wetu tunaoutumia wa ‘online registration system’ lakini kuna mpango ambao utatuwezesha ili mifumo hii iweze kusomana na ikisomana urasimu utaondoka kwa watu tunaowahudumia,” amesema Roida.

Kwa upande wake Kigahe amesema licha ya kuwapo kwa changamoto ya mtandao lakini kuna maboresho makubwa Brela na kuitaka kuendelea kushirikiana na taasisi nyingine kurahisisha utoaji huduma.

“Malalamiko makubwa yako kwenye leseni daraja B ambazo zinatolewa na halmashauri, muendelee kuboresha mifumo ili wananchi wasipate vikwazo katika kufanya biashara…tuone namna ya kuiboresha mifumo yetu ili isomane,” amesema Kigahe.

Katika maonesho hayo Brela ina mabanda mawili ambapo wanatoa huduma za papo kwa papo na kuwapatia usaidizi wale waliokwama kujisajili kwa njia ya mtandao.

Huduma hizo zinahusisha usajili wa majina ya biashara, kampuni, utoaji wa leseni za biashara kundi 'A', leseni za viwanda na usajili wa viwanda vidogo.

Powered by Blogger.