KCU YATENGA MILIONI 950 KUANZISHA SACCOS


Mwenyekiti wa Bodi ya KCU, Ressy Mashulano (Wakwanza kushoto), akiwaeleza wananchi shughuli wanazofanya walipotembelea banda lao lililopo Kijiji cha Ushirika kwenye Maonesho ya Nanenane Kitaifa viwanja vya John Mwakangale, jijini Mbeya.


Na Nora Damian, Mbeya

Chama Kikuu cha Ushirika Mkoa wa Kagera (KCU 1990 Ltd) kimetenga Sh milioni 950 kwa ajili ya kuanzisha vyama vya ushirika wa akiba na mikopo (Saccos) ili kusaidia wakulima wa kahawa. 

Chama hicho kina jumla ya vyama vya ushirika vya msingi (Amcos) 141 na wanachama 70,000.

Akizungumza Agosti 4, 2023 kwenye banda lao lililopo Kijiji cha Ushirika katika Maonesho ya Nanenane Kitaifa viwanja vya John Mwakangale, jijini Mbeya, Mwenyekiti wa Bodi ya KCU, Ressy Mashulano, amesema hatua hiyo inalenga kuwawezesha wakulima wa kahawa kupata mikopo nafuu na kuondokana na tabia ya kuuza kahawa kwa njia zisizo rasmi maarufu kama ‘Obutura’.   

“Maandalizi ya kuanzisha saccos yako kwenye hatua za mwanzo lakini tunategemea kufikia mwishoni mwa Novemba mwaka huu itakuwa tayari imeanza,” amesema Mashulano.


Mwenyekiti wa Bodi ya KCU, Ressy Mashulano (kushoto), akimweleza Katibu Tawala wa Mkoa wa Rukwa, Gerald Kusaya, shughuli wanazofanya baada ya kutembelea banda la chama hicho lililopo Kijiji cha Ushirika kwenye Maonesho ya Nanenane Kitaifa viwanja vya John Mwakangale, jijini Mbeya.

Amesema pia msimu ulioisha wamefanikiwa kurudisha faida kwa wakulima Sh milioni 641 na kutenga zaidi ya Sh milioni 950 kwa ajili ya kuanzia Saccos.

Amesema hivi sasa wanaendesha minada ya moja kwa moja Bukoba na kahawa nyingine hupelekwa katika mnada wa Moshi.

Mwenyeiti huyo amesema wanatoa elimu kwa umma na kuhamasisha unywaji wa kahawa ufikie angalau asilimia 30 ili kukuza soko la ndani.

“Ni tabia na kasumba tangu zamani wenzetu waliokuwa na mashamba ya chai walikuwa wanawaambia watu kwamba kahawa inaleta presha, lakini si kweli…mimi kila siku nakunywa kahawa sijapata matatizo,” amesema.

Meneja Mauzo ya Nje ya Nchi wa KCU, Josephat Sylvand, amesema mwelekeo wa bei ya kahawa ni mzuri ambayo haijawaji kutokea kwa miaka 15 iliyopita.

Amesema kwa Kagera wanalima zaidi kahawa aina ya Robusta kwa kuwa ina tabia ya kupenda sehemu zenye mwinuko wa chini. 


Powered by Blogger.