WANAFUNZI NIT WABUNI MASHINE KUSAIDIA WAKULIMA, WAFUGAJI



Mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Hytham Kerenge, akionesha mashine ya kusaga nafaka inayowawezesha wajasiriamali kuzalisha chakula kwa wingi.


Na Nora Damian

Wanafunzi wa mwaka wa nne wa shahada ya uhandisi wa mitambo katika Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) wamebuni mashine zinazowasaidia wakulima na wafugaji kuzalisha chakula kwa muda mfupi na kwa gharama nafuu.

Mashine hizo na wanafunzi waliozibuni kwenye mabano ni ya kukamua masega ya asali (Princess Kabona), kuchakata chakula cha mifugo (Adventina Stambuli) na kusaga nafaka (Hytham Kerenge).

Akizungumza Jumatano Agosti 2, 2023 kwenye Maonesho ya Kilimo ya Nanenane ambayo kitaifa yanafanyika katika viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya, Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Atupele Mwakibete, amewapongeza kwa ubunifu huo kwani mashine hizo zitarahisisha maisha ya Mtanzania.

“Nimefurahi kuona chuo kimepiga hatua, miaka ya 2005 kurudi nyuma hakikuwa hivi, kilikuwa na wanafunzi wachache wasiosidi 500. Leo kina wanafunzi zaidi ya 12,000 ambao wanapata mafunzo na kozi mbalimbali.

“Vijana hawa wawe mfano kwa mabinti wengine kwamba wanaweza, zama za zamani kwamba mtoto wa kike hawezi zilishapitwa na wakati,” amesema Mwakibete.


Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Atupele Mwakibete (kushoto), akizungumza na wanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji, Adventina Stambuli na Hytham Kerenge (kulia) waliobuni mashine kusaidia wakulima na wafugaji.

Naye Adventina amesema mashine aliyobuni inawezesha wafugaji wadogo kuzalisha chakula kingi cha mifugo kwani inachakata kilo 100 kwa saa na kumpunguzia gharama za kuzalisha na muda.

“Niligundua katika jamii mashine nyingi zilizopo zinafanya kazi moja hivyo, nilibuni mashine hii inayofanya zaidi ya kazi moja ili kumrahisishia mkulima kutumia gharama ndogo na muda mchache,” amesema Adventina.

Hytham aliyebuni mashine ya kusaga nafaka amesema inawawezesha wajasiriamali wa kati kuzalisha chakula kwa wingi ambapo inasaga na kuchanganya kilo 20 kwa saa.

Princess aliyebuni mashine ya kukamua masega ya asali amesema inawawezesha wajasiriamali wadogo na wa kati kukamua masega ya asali kwa ufanisi zaidi ambapo inakamua lita 50 kwa saa.

Amesema mashine hiyo ni rahisi kutumia na inaweza kutumika bila nishati ya umeme.

Ofisa Uhusiano wa chuo hicho, Juma Mandai, amesema wanafunzi kabla ya kumaliza masomo hutakiwa kutengeneza vitu mbalimbali ambavyo huvibuni kwa lengo la kusaidia jamii kutatua changamoto mbalimbali.

“Kwenye maonesho haya tunaonyesha mashine hizi kwa wadau ambao wangependa kujiendeleza katika fani mbalimbali ikiwemo uhandisi,” amesema Mandai.



Powered by Blogger.