DNA KUBAINI WABAKAJI, WALAWITI NDANI YA SAA 72


Meneja wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Elias Mulima, akizungumza na waandishi wa habari katika Maonesho ya Kilimo Nanenane viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya.


Na Nora Damian, Mbeya

Saa 72 zinatosha kwa teknolojia ya uchunguzi wa vinasaba (DNA) kubaini mtu aliyetenda kitendo cha ubakaji au ulawiti, imeelezwa.

Takwimu za mwaka 2021 za Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Makundi Maalumu zinaonesha watoto 11,499 walifanyiwa ukatili na kati yao 5,899 walibakwa na 1,114 walilawitiwa.

Kwa Zanzibar takwimu za karibuni zilizotolewa na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto zinaonesha kwa kipindi cha kuanzia 2017 hadi 2022 matukio 6,461 yameripotiwa yakiwemo ya ubakaji na ulawiti.

Akizungumza na waandishi wa habari katika Maonesho ya Kilimo Nanenane ambayo kitaifa yanafanyika katika viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya, Meneja wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Elias Mulima, amesema teknolojia hiyo ina uwezo wa kubaini mtu alitenda ubakaji au ulawiti.

“Aliyefanyiwa tukio la ubakaji anatakiwa atoe taarifa haraka jeshi la polisi, kisha atapelekwa kwa daktari ili aweze kuchukuliwa sampuli…ndani ya saa 72 inabidi mambo yote yafanyike.

“Tunasisitiza sana tukio linapotokea aende haraka polisi kwa sababu wakati mwingine mtu anaweza kubakwa halafu anakwenda kuripoti polisi baada ya wiki, sampuli ambazo zingefaa kuthibitisha muhusika haziwezi kupatikana,” amesema Mulima.


Mkazi wa Mbeya akipata maelezo kutoka kwa Ofisa wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Georgina Kilindo (kulia), alipotembelea banda la mamlaka hiyo.

Meneja huyo amehimiza jamii kuripoti matukio ya ubakaji na ulawiti ndani ya saa 72 kuwezesha sampuli kupatikana kirahisi.

Aidha amesema DNA ina kazi nyingi kwani wamekuwa wakipokea sampuli kutokana na kesi za mirathi kuthibitisha uhalali wa watoto wanaojitokeza pindi inapotokea mzazi amefariki.

“DNA inatumika kutambua koo au ndugu, inatumika kwenye uchunguzi wa kesi ambazo baba wametekeleza watoto na kukataa kutoa matunzo, hivyo hufanyika kuthibitisha kama kweli ni mtoto wake.

“Inatumika kwenye majanga kama ya moto, ajali za majini, kuna miili inaokotwa haitambuliki, au mifupa mtu amefariki haijulikani ndugu zake DNA inafanyika kuweza kutambua,” amesema.

Meneja huyo amesema teknolojia hiyo pia huweza kusaidia watu waliosingiziwa matukio mbalimbali kama ya mauaji au ubakaji.







Powered by Blogger.