MAJALIWA AZITAKA BENKI KUPUNGUZA RIBA MIKOPO YA WAKULIMA


Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa (kushoto), akimsikiliza Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, baada ya kukagua mabanda ya Maonesho ya Nanenane Kitaifa kwenye viwanja vya John Mwakangale, jijini Mbeya.


Na Nora Damian, Mbeya

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameziagiza benki kupunguza riba zaidi katika mikopo ili kuwasaidia wakulima, wafugaji na wavuvi.

Kwa sasa benki nyingi zinatoa mikopo katika sekta ya kilimo kwa riba ya asilimia tisa ambayo imeshuka kutoka asilimia 13 iliyokuwepo awali.

Ametoa maagizo hayo Alhamisi Agosti 3, 2023 baada ya kukagua mabanda ya Maonesho ya Nanenane Kitaifa kwenye viwanja vya John Mwakangale, jijini Mbeya.

“Nimepitia mabanda ya mabenki na kuwauliza kuhusu riba, wengi wao wameshusha kutoka asilimia 12 au 13 ya awali na wamefika asilimia tisa…Naibu Gavana wape miongozo ili wakulima wetu wapate nafuu,” amesema Majaliwa.

Aidha ameitaka Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) kuendelea kufungua matawi hasa katika Mikoa ya Rukwa, Iringa na Ruvuma na kuongeza kasi ya utoaji huduma kuwafikia wakulima wengi zaidi.

Pia amezitaka Wizara ya Kilimo na Wizara ya Mifugo na Uvuvi ziandae utaratibu wa kuziweka kwenye mifumo rahisi na kuzifikisha kwa wakulima na wavuvi maelezo juu ya upatikanaji wa mitaji, kupata pembejeo kwa urahisi na kuifikia teknolojia mpya.

Waziri Mkuu amesema maonesho ya mwaka huu ni mazuri zaidi ya mwaka jana kwani kuna teknolojia nyingi mpya ambazo zimebuniwa na vijana.

“Kama tutaendelea kulima na kufuga hivi tunaweza kusema sasa sekta ya kilimo imeanza kwenda kwenye mwelekeo mzuri. Tanzania iko vizuri kijiografia na imekaa kimkakati, kwa hiyo tukiwa na uzalishaji mzuri wa chakula na mazao ya kibiashara, tukafuga kibiashara na kuvua kibiashara tutaweza kulisha nchi jirani na wakulima wenyewe wataweza kunufaika,” amesema.

Amesema Rais Samia aliongeza bajeti za wizara hizo ambapo kilimo imefikia Sh bilioni 900 na kuwaasa Watanzania kuingia kwenye biashara ya ufugaji.

“Vijana waliojiunga na mpango wa BBT walioanza mafuzo mwaka huu, wamekaribia kuhitimu. Eneo la BBT liko pia kwenye mifugo. Unaweza kupewa eneo, ukaweka mifugo na kuwanenepesha, kubwa zaidi ni upatikanaji wa mitaji,” amesema.

Kuhusu ushirika, Waziri Mkuu amemtaka Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, asimamie usajili, mapato, matumizi na mwenendo wa AMCOS ili ziweze kuleta tija kwa wakulima.

Awali Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega, amesema wamedhamiria kuwatumia vijana hivyo wataingia mkataba wa makubaliano na Jeshi la Kujenga Taifa ili asilimia 40 ya vijana watoke jeshini, asilimia 30 iwe ni wataalamu wao na asilimia 30 iwe ni vijana kutoka maeneo mengine ya asili.


Waziri wa Mifugo na Uvuvi. Abdallah Ulega, akizungumza na mmoja wa vijana wakati alipokuwa akikagua mabanda ya Maonesho ya Nanenane Kitaifa kwenye viwanja vya John Mwakangale, jijini Mbeya.

“Tuna banda kubwa kwenye maonesho haya ambalo wanatumia vijana kuonesha teknolojia ya kunenepesha mifugo ili kusaidia kubadilisha mtazamo wa wafugaji nchini,” amesema Ulega.

Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, amesema hai ya uzalishaji chakula nchini ni nzuri kwani mikoa ya uzalishaji imeongezeka kutoka mitano ya awali hadi 13.

“Sasa hivi tuna mikoa 13 ya uzalishaji wa chakula nchini na mwaka huu imezalisha zaidi ya asilimia 70 ya chakula chote nchini,” amesema Bashe.



Powered by Blogger.