SHERIA USIMAMIZI WA MAAFA YAPIGIWA CHAPUO
Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Menejimenti ya Maafa, Charles Msangi, akimweleza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, kuhusu shughuli zinazofanywa na idara hiyo alipoitembelea katika Maonesho ya Nanenane Kitaifa viwanja vya John Mwakangale, jijjni Mbeya.
Na Nora Damian, Mbeya
Idara, taasisi za serikali na wadau wa sekta binafsi wametakiwa kuhakikisha wanafahamu majukumu yao kupitia sheria ya usimamizi wa maafa ya mwaka 2022 na kanuni zake ili kuzuia au kupunguza majanga nchini.
Akizungumza Agosti 3, 2023 kwenye Maonesho ya Nanenane ambayo kitaifa yanafanyika viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya, Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Menejimenti ya Maafa, Charles Msangi, amesema lengo ni kuhakikisha majanga yanazuiliwa yasilete madhara kwa binadamu.
Msangi alikuwa akizungumza wakati Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alipotembelea idara hiyo ambayo ni mojawapo katika ofisi yake.
“Tunatoa elimu kwa umma hasa kuhusu sheria ya usimamizi wa maafa ya mwaka 2022 na kanuni zake za mwaka 2022. Tunaeleza kuhusu mkakati wa taifa wa usimamizi wa maafa pamoja na miongozo na mipango ya shughuli za usimamizi wa maafa,” amesema Msangi.
Amesema muundo wa uratibu na usimamizi wa maafa unaanzia ngazi ya taifa ambapo kuna kamati ya usimamizi wa maafa, ngazi ya mkoa, wilaya hadi Kijiji.
“Lengo kubwa ni kutoa elimu kuhusu mfumo na muundo ambao unashughulika na shughuli za usimamizi wa maafa ambazo zimejikita kuanzia hatua za awali za kuzuia na kupunguza madhara ya majanga,” amesema.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akiangalia majarida mbalimbali alipotembelea banda la idara ya maafa katika Maonesho ya Nanenane Kitaifa viwanja vya John Mwakangale, jijjni Mbeya.
Amefafanua kuwa yako majanga yanayosababishwa na shughuli za asili kama matetemeko na mafuriko ambayo hayawezi kuzuilika lakini hatua zinaweza kufanyika kupunguza madhara au athari zake.
Amefafanua kuwa yako majanga yanayosababishwa na shughuli za asili kama matetemeko na mafuriko ambayo hayawezi kuzuilika lakini hatua zinaweza kufanyika kupunguza madhara au athari zake.
Kulingana na mkurugenzi huyo, majanga mengine husababishwa na shughuli za binadamu ambayo yanaweza kuzuilika.
Amesema wana mkakati wa kutoa elimu kwa mwananchi mmoja mmoja kwa sababu suala la usimamizi wa maafa linaanza na mtu binafsi.
“Tunatoa miongozo kwa majanga mbalimbali ambayo yanatokea mara kwa mara nchini, mfano mafuriko sababu zake zinazuilika au zinaweza kupunguza madhara kama kuhakikisha wananchi wanakaa katika maeneo salama na kuhakikisha mazingira yanakuwa safi,” amesema Msangi.
Idara hiyo imeandaa vipeperushi vyenye lugha nyepesi kuhusu majanga mbalimbali na wajibu wa mtu mmoja mmoja na namna anavyoweza kushiriki kuhakikisha anapunguza au kuzuia majanga yasilete madhara kwa binadamu.

