NMB YAKOPESHA WAKULIMA TRILIONI 1.61
Meneja wa NMB Kanda ya Nyanda za Juu, Straton Njau (kushoto), akieleza huduma zinazotolewa na benki hiyo kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alipotembelea banda la benki hiyo kwenye Maonesho ya Nanenane Kitaifa viwanja vya John Mwakangale, jijini Mbeya.
Na Mwandishi Wetu, Mbeya
Benki ya NMB imetoa mikopo ya riba nafuu yenye thamani ya zaidi ya Sh trilioni 1.61 katika sekta ya kilimo katika kipindi cha miaka sita.
Aidha benki hiyo pia imedhamini Maonesho ya Kilimo (Nanenane) kwa Sh milioni 486 katika kipindi cha miaka minne.
Akizungumza Agosti 3, 2023 kwenye Maonesho ya Kilimo Nanenane ambayo kitaifa yanafanyika viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya, Meneja wa NMB Kanda ya Nyanda za Juu, Straton Njau, amesema hiyo ni uthibitisho wa utayari na uimara wao katika kuhudumia sekta ya kilimo nchini.
Njau alikuwa akizungumza wakati Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alipotembelea banda hilo kujionea huduma mbalimbali wanazozitoa.
"Lengo la benki yetu ni kuunga mkono juhudi za Serikali za kujenga mazingira wezeshi kwa sekta ya kilimo na kuongeza mchango wake kwa Pato la Taifa," amesema Njau.
Amesema mikopo hiyo ilielekezwa katika mazao ya kimkakati ya tumbaku, chai, alizeti, kahawa, mpunga, mahindi, zabibu, mihogo, zana za kilimo na vitendea kazi kwenye nyanja za uvuvi na ufugaji.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akifurahia jambo na Meneja wa NMB Kanda ya Nyanda za Juu, Straton Njau, alipotembelea banda la benki hiyo kwenye Maonesho ya Nanenane Kitaifa viwanja vya John Mwakangale, jijini Mbeya.
Mwaka huu NMB imedhamini maonesho hayo kwa Sh milioni 80 na kufanya udhamini wa taasisi hiyo kufikia Sh milioni 255 katika kipindi cha miaka minne.
"Tumedhamiria kuwainua kiuchumi wadau wa kilimo, NMB ndio benki ya kwanza nchini sio tu kukopesha kiasi kikubwa, bali pia kushusha riba kwa mikopo ya kilimo, uvuvi na ufugaji hadi kufikia asilimia 9, kwa mikopo hiyo inayoanzia Sh. 200,000 hadi Sh bilioni 1 kwa mtu mmoja mmoja, vikundi, taasisi, mashirika na vyama vya ushirika vya wakulima (AMCOS)," amesema.
Kwa mujibu wa Njau, ndani ya miaka miwili NMB imetenga Sh bilioni 20 kwa ajili ya ujenzi wa maghala ya mazao vijijini ili kukabiliana na upotevu na uharibifu wa mazao ambapo tayari zaidi ya Sh bilioni 7 kati ya hizo zimeshakopeshwa mwaka huu pekee.
Amesema pia wametenga Sh bilioni 20 kuwezesha Program ya Kuandaa Vijana na Wanawake kwa Kesho Iliyo Bora (BBT) na mchakato wa kukamilisha hilo unaendelea baina yao na wizara ya kilimo.
Amewapongeza wakulima wa parachichi, kahawa, mpunga na mahindi Mkoa wa Mbeya kwa kufungua zaidi ya akaunti 87,044 ambazo ni kati ya akaunti 644,034 zilizofunguliwa na wakulima wote nchini katika kipindi cha miaka miwili.
Njau amesema pia kupitia NMB Foundation wametoa elimu ya fedha na mafunzo ya biashara kwa AMCOS 1,450 nchini nzima zikiwemo 555 za wakulima wa Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini pamoja na mkulima mmoja mmoja wapatao 233,087 kote Tanzania.
Amesema lengo ni kuwajengea uwezo wa namna bora ya kusimamia mapato yao.
Benki hiyo imeahidi neema kwa wadau wa mnyororo wa thamani wa kilimo hususani wakulima.

