‘UKIONA BANGI SHAMBANI NG’OA’
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini katika Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Florence Khambi, akionesha mmea wa bangi kwenye Maonesho ya Kilimo ya Nanenane Kitaifa yanayofanyika viwanja vya John Mwakangale, jijini Mbeya.
Na Nora Damian, Mbeya
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imewaasa wakulima kung’oa mimea ya bangi inayoota shambani ili kudhibiti uzalishaji na matumizi ya dawa hizo.
Taarifa ya hali ya dawa za kulevya ya mwaka 2022 iliyotolewa na mamlaka hiyo hivi karibuni inaonesha bangi imeendelea kuwa dawa ya kulevya inayolimwa na kutumiwa kwa wingi ambapo hekari 179 za mashamba ya bangi ziliteketezwa na tani 20.58 zilikamatwa.
Kulingana na taarifa hiyo watuhumiwa 10,277 wakiwemo wanaume 9,549 na wanawake 728 walikamatwa.
Aidha katika mwaka huo watuhumiwa watatu walikamatwa wakihusishwa na usambazaji wa bidhaa zilizotengenezwa kwa kuhusisha bangi kama vile biskuti, asali, majani ya chai na keki.
Mamlaka hiyo inatumia Maonesho ya Kilimo ya Nanenane Kitaifa yanayofanyika viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya kuonesha dawa halisi za kulevya ukiwemo mmea wa bangi ili wananchi waufahamu na kudhibiti uzalishaji na usambazaji wake.
Akizungumza na waandishi wa habari Jumatano Agosti 2, 2023 Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini DCEA, Florence Khambi, amesema katika maonesho hayo wananchi wanapata fursa ya kuziona dawa halisi za kulevya na kuelimishwa madhara yake.
“Tunatoa elimu kwa wananchi na kuwaonesha dawa za kulevya ukiwemo mmea wa bangi ili waweze kuutambua. Mmea wa bangi ni uoto wa asili ambao unaweza kuota sehemu yoyote hata pembeni mwa nyumba, mwananchi akiuona anatakiwa aung’oe.
“Asipoung’oa mbegu yake ikikomaa inaweza kusambaaa na kuendelea kuota katika maeneo mbalimbali hasa mashambani mbegu zinaweza kusafirishwa kwa maji,” amesema Khambi.
Ofisa wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Shabani Miraji, akitoa elimu kwa mkazi wa Mbeya aliyetembelea banda la mamlaka hiyo katika Maonesho ya Nanenane Kitaifa viwanja vya John Mwakangale, jijini Mbeya.
Amesema pia wananchi wanaelimishwa kuhusu biashara ya dawa za kulevya zinazoingizwa nchini jinsi zinavyofungwa na kusafirishwa ili waweze kushiriki katika mapambano ya kudhibiti biashara hiyo.
“Wananchi watembelee banda letu wapate elimu kuhusiana na madhara ya dawa za kulevya, waone dawa halisi za kulevya kwa sababu wengine wanaweza kujikuta wanaingia kwenye matatizo bila kujua,” amesema.
Amesema pia wananchi wanaelimishwa kuhusu biashara ya dawa za kulevya zinazoingizwa nchini jinsi zinavyofungwa na kusafirishwa ili waweze kushiriki katika mapambano ya kudhibiti biashara hiyo.
“Wananchi watembelee banda letu wapate elimu kuhusiana na madhara ya dawa za kulevya, waone dawa halisi za kulevya kwa sababu wengine wanaweza kujikuta wanaingia kwenye matatizo bila kujua,” amesema.

