UPANDIKIZAJI ULOTO SULUHISHO WATOTO WENYE SIKOSELI


Mtoto Elisha Osena (kulia), aliyepandikizwa uloto katika Hospitali ya Benjamin Mkapa. Kushoto ni dada yake, Esther Osena ambaye alitolewa uloto huo. Huduma hiyo ilizinduliwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwenye hospitali hiyo Mei 10, 2023.


Na Nora Damian, Mbeya

Wazazi wenye watoto wenye ugonjwa wa sikoseli wametakiwa kuwapeleka katika vituo vya afya wapatiwe huduma ikiwemo ya upandikizaji uloto.

Huduma hiyo ilizinduliwa katika Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) Mei, 2023 na kuifanya Tanzania kuwa nchi ya sita Afrika kuianzisha na ya kwanza Afrika Mashariki na Kati.

Akizungumza Agosti 2, 2023 kwenye Maonesho ya Nanenane Kitaifa viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Damu katika hospitali hiyo, Stella Malangahe, amesema upandikizaji uloto unalenga kuondoa kabisa matatizo ya sikoseli.

“Mtoto akizaliwa na sikoseli kama akiwa na vigezo vya kupatiwa huduma hii na akapatiwa, tunategemea ugonjwa utaondoka kabisa katika mwili wake,” amesema Dk Malangahe.

Amesema huduma hiyo ilianza rasmi mwaka huu na mpaka sasa wameshapandikiza watoto wanne waliokuwa na tatizo hilo.

Kwa mujibu wa daktari huyo, sikoseli ni ugonjwa wa kurithi ambao mtoto hupata kutoka kwa baba na mama kwa kurithi vinasaba vibovu ambavyo hutengeneza chembechembe nyekundu ya damu ambayo huwa na hitilafu.


Mtaalam wa upimaji wa uono na miwani kutoka Hospitali ya Benjamin Mkapa, Godfrey Felix, akimpima mteja aliyetembelea banda la hospitali hiyo katika Maonesho ya Kitaifa ya Nanenane viwanja vya John Mwakangale,

jijini Mbeya.

Amesema hali hiyo husababisha damu kushindwa kusafirishwa vizuri na mtoto husika hukabiliwa na upungufu wa damu wa mara kwa mara, homa za mara kwa mara, maumivu makali katika viungo vya mwili na athari za muda mrefu kama uharibifu wa figo, ini, mapafu, ubongo na kuwa na hatari ya kupata kiharusi.

“Anapokuwa katika umri wa kupata mtoto anakuwa hana uwezo wa kupata mtoto vizuri kama ambavyo watu wengine wanapata. Hulazwa hospitali mara kwa mara na kumfanya mzazi kutumia gharama na muda mrefu kumhudumia,” amesema.

Ofisa Uhusiano wa hospitali hiyo, Raymond Mtani, amesema katika maonesho hayo wanatoa elimu ya huduma za matibabu ya ubingwa bobezi kama vile upandikizaji wa figo, uloto, macho, pua, sikio na koo.

Amefafanua kuwa kwa wenye matatizo ya pua, koo na masikio pamoja na macho watatibiwa bure na madaktari bingwa wa magonjwa hayo ambao wapo kwenye banda la hospitali hiyo.



Powered by Blogger.