VYAMA VYA USHIRIKA VYAASWA KUTUMIA TEHAMA KUZUIA UHALIFU
Ofisa Masoko wa Kampuni ya Tehama (VeriDoc Global), Swamiath Tizetwa (katikati), akimweleza Katibu Tawala wa Mkoa wa Rukwa, Gerald Kusaya, shughuli wanazozifanya wakati alipotembelea Kijiji cha Ushirika kwenye Maonesho ya Nanenane Kitaifa viwanja vya John Mwakangale, jijini Mbeya.
Na Nora Damian, Mbeya
Vyama vya ushirika vimetakiwa kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) kuzuia uhalifu wa mtandao na udukuzi wa nyaraka na bidhaa.
Ushauri huo umetolewa na Kampuni ya Tehama (VeriDoc Global) inayojenga mifumo ya kiusalama wa nyaraka, bidhaa na mnyororo wa ugavi kwa kutumia teknolojia ili kuzuia uhalifu wa kimtandao na udukuzi wa nyaraka na bidhaa.
Akizungumza Agosti 4, 2023 kwenye Maonesho ya Nanenane Kitaifa viwanja vya John Mwakangale, jijini Mbeya, Ofisa Masoko wa kampuni hiyo, Swamiath Tizetwa, amesema wanashirikiana na Shirikisho la Vyama vya Ushirika kutoa suluhisho bora la mnyororo wa ugavi kwa kutumia teknolojia ya ‘blockchain’ na misimbo salama ya ‘QR Codes’.
“Tunauza vifaa vya Tehama kwenye vyama vya ushirika zikiwamo simu za mkononi, printa, kompyuta mpakato na mizani pamoja na kutoa elimu ya tehama kwa vyama.
“Mfumo wetu unahakikisha unachukua kumbukumbu ya makabidhiano ya kidigitali, kila hatua ya mnyororo wa ugavi ambayo inaonesha mud ana mahali bidhaa inapopelewa," amesema Tizetwa.
Amesema kazi kubwa wanazofanya katika vyama vya ushirika ni kusaini mikataka ya kidigitali na kuweka alama za utambuzi kwenye nyaraka zao.
Kwa mujibu wa Tizetwa, kazi nyingine ni kutoa suluhisho la vifungashio na kuweka alama za utambuzi kwenye bidhaa zao.
Amesema wanatoa mifumo ya mahesabu kwa vyama vya kuweka akiba na mikopo Saccos na vyama vya msingi Amcos.
