CRDB YAWEZESHA VIJANA, WANAWAKE 45,000


Meneja wa Benki ya Crdb Kanda ya Nyanda za Juu, Jenipher Tondi, akimkabidhi zawadi Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alipotembelea banda la benki hiyo katika Maonesho ya Nanenane Kitaifa viwanja vya John Mwakangale, jijini Mbeya.

Na Nora Damian, Mbeya

Benki ya CRDB imesema imeanza kutekeleza kwa vitendo kaulimbiu ya Maonesho ya Kilimo ya Nanenane 2023 kwa kuwapa mafunzo na mtaji wezeshi vijana na wanawake 45,000 nchi nzima.

Kaulimbiu ya Maonesho ya Nanenane 2023 ambayo kitaifa yanafanyika viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya inasema ‘Vijana na wanawake ni msingi imara wa mifumo endelevu ya chakula’.

Akizungumza Agosti 3, 2023 kwenye maonesho hayo Meneja wa benki hiyo Kanda ya Nyanda za Juu, Jenipher Tondi, amesema vijana na wanawake wanapatiwa mafunzo ya elimu ya fedha kisha mtaji wezeshi.

Tondi alikuwa akizungumza wakati Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alipotembelea banda la benki hiyo kwenye maonesho hayo.

“Tumeanza kutekeleza kwa vitendo kaulimbiu ya maonesho ya 2023, tumeanza kutoa elimu kwa vijana na wanawake na kuboresha biashara zao ambazo ni changamoto,” amesema Tondi.


Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akifurahia jambo na Waziri wa Kilimo. Hussein Bashe (katikati) na Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson baada ya kutembelea banda la benki ya Crdb katika Maonesho ya Nanenane Kitaifa viwanja vya John Mwakangale, jijini Mbeya.

Benki hiyo inatekeleza program ya Imbeju (Mtaji Wezeshi kwa Vijana) kwa kutoa mikopo ambayo haina riba kuanzia Sh 200,000 hadi Sh milioni 30 ambazo hurejeshwa hadi miezi 24

Amesema pia wataendelea kutoa elimu ya fedha kwa vijana walio katika program ya Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT) katika vituo mbalimbali atamizi vya mradi huo.

Kwa mujibu wa meneja huyo benki hiyo imetoa mikopo katika sekta ya kilimo zaidi ya Sh trilioni 1.3 ambapo Sh bilioni 494 zilielekezwa katika mazao makuu ya kimkakati na kuvinufaisha vyama vya ushirika 472.

Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, amesema benki za ndani ikiwemo CRDB zimeendelea kuunga mkono sekta ya kilimo na mifugo na kwamba wako kwenye mazungumzo na benki hiyo ili kupata uungwaji mkono katika programu ya BBT.

Waziri Mkuu, Majaliwa ameipongeza benki hiyo kwa kuunga mkono juhudi za serikali za kumkwamua mkulima na mfugaji kupitia mikopo mbalimbali wanayoitoa.



Powered by Blogger.