KCBL YAKUZA MTAJI KWA BILIONI 6, KUSAYA AIPIGIA DEBE


Mkuu wa Kitengo cha Mikopo na Biashara Benki ya Ushirika Kilimanjaro, Frank Wilson, akimweleza Katibu Tawala wa Mkoa wa Rukwa, Gerald Kusaya, huduma wanazotoa baada ya kuwatembelea kwenye Maonesho ya Nanenane Kitaifa viwanja vya John Mwakangale, jijini Mbeya. Kulia ni Meneja Mkuu wa KCBL, Godfrey Ng'ura.

Na Nora Damian, Mbeya
 
Benki ya Ushirika Mkoa wa Kilimanjaro (KCBL) imeongeza mtaji wa zaidi ya Sh bilioni 4 katika kipindi cha miaka miwili na kufikia Sh bilioni 6.
 
Benki hiyo ina malengo ya kufikisha mtaji wa Sh bilioni 15 ifikapo Oktoba mwaka huu ili iweze kupata leseni ya kuwa benki ya taifa ya ushirika.
 
Katibu Tawala wa Mkoa wa Rukwa, Gerald Kusaya, ambaye ametembelea banda la benki hiyo leo Ijumaa Agosti 4, 2023 amesema wanaushirika wanapaswa kujivunia kuwapo kwa benki hiyo.
 
Banda la benki hiyo lipo katika Kijiji cha Ushirika kilichopo Maonesho ya Nanenane Kitaifa viwanja vya John Mwakangale, jijini Mbeya ambacho kinaratibiwa na Tume ya Maendeleo ya Ushirika (TCDC).
 
“Wanaushirika mpende benki yenu ya KCBL kwa sababu ndio mkombozi kwa wanaushirika. Mwanaushirika yeyote lazima ajivunie kwamba anacho cha kwake…nategemea wana ushirika popote walipo nchini waweze kujiunga na benki hii,” amesema Kusaya.


Katibu Tawala wa Mkoa wa Rukwa, Gerald Kusaya, akiangalia tumbaku baada ya kutembelea banda la Chama Kikuu cha Ushirika cha Wakulima wa Tumbaku Chunya kwenye Maonesho ya Nanenane Kitaifa viwanja vya John Mwakangale, jijini Mbeya.
 
Amesema wanaushirika wengi wakijiunga watawezesha mtaji wa benki hiyo kuongezeka haraka na kutoa wito kwa viongozi kufungua matawi zaidi mikoani.
 
Kusaya amesema pia kuna mabadiliko makubwa katika sekta ya ushirika ambao unakua ukilenga kumkomboa zaidi mwana ushirika.
 
“Maendeleo ya nchi hii yatatokana na ushirika, nimefurahishwa na wazo la kuwa na Kijiji cha Ushirika, ni eneo moja ambalo linaunganisha ushirika kwa pamoja,” amesema Kusaya.
 
Mkuu wa Kitengo cha Mikopo na Biashara KCBL, Frank Wilson, amesema mwitikio wa watu kujiunga na benki hiyo ni mkubwa hatua iliyosaidia kuongeza mtaji wa zaidi ya Sh bilioni 4 kwa miaka miwili.
 
“Benki hii ni kiungo muhimu kwa wakulima, tumekuwa tukiwawezesha wakulima kupitia vyama vya ushirika na mtu binafsi…tuko kwenye mchakato wa kuifanya kuwa benki ya taifa ya ushirika ili kutanua wigo wa kuwahudumia wakulima wengi zaidi,” amesema Wilson.
 
Amesema pia katika mwaka 2022/23 benki hiyo imekopesha zaidi ya Sh bilioni 3 na kati ya hizo Sh bilioni 1 walikopeshwa vijana na wanawake wanaojihusisha na kilimo.
 
Vijana na wanawake wanaojihusisha na kilimo wamekuwa wakiwezeshwa kununua mazao, kupata pembejeo za kilimo na masoko.

Aidha amesema wateja si lazima wawe wana ushirika kwani watu mbalimbali wanaweza kuwekeza katika benki hiyo pamoja na watumishi wa umma ambao mpaka sasa wamekopeshwa Sh bilioni 2.6.


Powered by Blogger.