BRELA YATAJA MANUFAA KURASIMISHA BIASHARA


Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano kutoka Wakala ya Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Roida Andusamile (kulia), akimkabidhi cheti cha usajili wa majina Joseph Nzunda, aliyefika katika banda lao kujisajili kwenye Maonesho ya Nanenane Kitaifa viwanja vya John Mwakangale, jijini Mbeya.

Na Nora Damian, Mbeya
 
Wakala wa Usajili ya Biashara na Leseni (BRELA) umewataka wananchi kubadilika na kuacha kufanya biashara kwa mazoeya badala yake wafuate taratibu na kurasimisha biashara.
 
Katika Maonesho ya Nanenane Kitaifa yanayoendelea viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya, wakala huo unatoa huduma za papo kwa papo za usajili wa majina ya biashara na kampuni.
 
Akizungumza Agosti 4, 2023 na waandishi wa habari Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano BRELA, Roida Andusamile, amesema serikali ina nia njema na wananchi kwani wanaporasimisha biashara inawawezesha kukua na kutambulika zaidi.
 
“Kilimo ni biashara hivyo wakulima watumie fursa inayotolewa na serikali kwa kuhakikisha wanarasimisha biashara zao kupitia usajili wa majina ya biashara, usajili wa kampuni, usajili wa alama za biashara na huduma, kupata leseni ya biashara kundi A na kupata leseni ya kiwanda.
 
“Mwingine haishii tu kulima anaweza kuwa na kiwanda cha kusaga nafaka kwahiyo viwanda vinatakiwa kupata leseni na kama ni kidogo kinatakiwa kusajiliwa,” amesema Roida.
 
Amesema usajili wa jina la biashara una faida nyingi zikiwemo kutambulisha na kukuza biashara husika, urahisi wa kupata mikopo katika taasisi za fedha na zabuni mbalimbali zinazotolewa serikalini na nyingine.


Watumishi wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), wakiwahudumia wananchi waliofika katika banda lao kujisajili kwenye Maonesho ya Nanenane Kitaifa viwanja vya John Mwakangale, jijini Mbeya.
 
Amesema katika maonesho mbalimbali wanayoshiriki yakiwemo ya Nanenane wanatoa huduma za papo kwa papo na kuwapatia usaidizi wale waliokwama kujisajili kwa njia ya mtandao ambapo hadi sasa zaidi ya watu 30 wamesajili majina ya biashara.
 
“Nawasihi wale wote waliokwama kusajili kwa njia ya mtandao wafike katika mabanda yetu ili waweze kusaidiwa na kupata vyeti vyao,” amesema.
 
Mkazi wa Mtwara aliyepatiwa huduma hiyo Joseph Nzunda, amesema anajishughulisha kuchataka mazao ya mafuta kwa kuuongezea thamani ufuta lakini alikuwa hajasajili jina la biashara.
 
“Kilichonisukuma kuja kusajili jina la biashara nataka kuifanya shughuli yangu iwe halali na iweze kujulikana nifanye kazi kwa uhuru na uwazi zaidi.
 
“Nawashauri watu wengine wafuate utaratibu wa kusajili majina ya biashara ili wawe huru zaidi kufanya shughuli zao,” amesema Nzunda.


Mkazi mwingine wa Mbeya aliyesajili jina la biashara, Bernard James, amesema huduma za Brela zinapatikana kwa haraka na kwa ufanisi na kuwashauri watu kujitokeza kusajili majina ya biashara.





Powered by Blogger.