CRDB YAKOPESHA TRILIONI 1.2 KWA WAKULIMA



Meneja Uhusiano Kilimo Biashara ofisi za Kanda Mbeya, Gilbert Kyando (kulia), akiwahudumia wateja katika banda la benki hiyo kwenye Maonesho ya Nanenane viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya.


Na Nora Damian, Mbeya

Benki ya CRDB imetoa mikopo ya zaidi ya Sh trilioni 1.2 ili kuwainua wakulima nchini na kuongeza uzalishaji.

Benki hiyo imepunguza riba ya mikopo kwa sekta ya kilimo na mnyororo wake wa thamani kutoka asilimia 20 hadi asilimia tisa pekee.

Akizungumza Jumatano Agosti 2, 2023 kwenye Maonesho ya Kilimo ya Nanenane ambayo kitaifa yanafanyika katika viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya, Meneja Uhusiano Kilimo Biashara ofisi za Kanda Mbeya, Gilbert Kyando, amesema benki hiyo inachangia asilimia 43 ya mikopo yote katika sekta ya kilimo nchini.

“Kwetu tunasema ni hatua kubwa ingawa tunaamini tuna kazi kubwa ya kufanya, mikopo mingi imekuwa ikitolewa katika hatua za juu za uchakataji, ununuzi na nyingine ambao hao wana nafuu kidogo kwa sababu hawakutani na changamoto za moja kwa moja kama anazokutana nazo mkulima.

“Mikopo yetu imewagusa wakulima wa kawaida na tunaamini katika ushirika kwa sababu ndiko kuna Watanzania wadogo wadogo wengi,” amesema Kyando.

Amesema mikopo hiyo imewanufaisha wakulima 7,059,400 kutoka katika vyama vya ushirika zaidi ya 472 nchi nzima.


Aidha amesema wamewekeza mtaji wa zaidi ya Sh bilioni 10.2 katika Benki ya Ushirika Kilimanjaro (KCBL Sh bilioni 7) na Benki ya Ushirika ya Tandahimba (TACOBA Sh bilioni 3.2) ambazo zilikuwa zinajiendesha kwa hasara.

Amesema pia kupitia program ya Imbeju (Mtaji Wezeshi kwa Vijana) wanatoa mikopo ambayo haina riba kuanzia Sh 200,000 hadi Sh milioni 30 ambazo hurejeshwa hadi miezi 24.

Kulingana na meneja huyo wanawake wanaohitaji mikopo hiyo wanapaswa kuwa kwenye vikundi wakati kwa vijana kuna dirisha maalumu lililopo katika kila halmashauri nchini linalowahudumia.

“Tunafahamu wanaojihusisha kwenye kilimo wengi ni wanawake na vijana na kupitia program hii tunawapa elimu ya msingi ya masuala ya fedha kabla mtu hajakopeshwa.

“Kikundi kinatakiwa kiwe na usajili wa miaka mitatu kwa sababu ni mikopo ambayo haina dhamana, wanawake wanasimamiana wao wenyewe na fedha anapewa mtu mmoja mmoja ili zisitumike vibaya,” amesema Kyando.







Powered by Blogger.