TSB KUONGEZA UZALISHAJI MKONGE
Watumishi wa Bodi ya Mkonge, Faith Kweka (katikati) na Ester Jonas (kulia) wakionesha bidhaa za mkonge kwa mwananchi aliyetembelea banda la bodi hiyo kwenye Maonesho ya Nanenane viwanja vya John Mwakangale jijjji Mbeya.
Na Nora Damian
Bodi ya Mkonge Tanzania (TSB) imesema imejipanga kuongeza uzalishaji wa mkonge kutoka tani 48,000 za sasa hadi kufikia tani 120,000 ifikapo mwaka 2025 ili kukidhi mahitaji ya soko la dunia.
Takwimu za 2021 za Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) zinaonesha mahitaji ya mkonge duniani ni zaidi ya tani 500,000.
Akizungumza na waandishi wa habari Agosti 2, 2023 katika Maonesho ya Kilimo Nanenane ambayo kitaifa yanafanyika katika viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya, Ofisa Uhusiano na Mawasiliano wa bodi hiyo, Esther Mbussi, amesema wameweka mikakati kufanikisha malengo hayo.
“Mwitikio wa wakulima ni mkubwa na zao la mkonge ni la kimkakati, kama sehemu ya maboresho ya uzalishaji wa zao hili nchini malengo tuliyonayo ni kuongeza uzalishaji hadi kufikia tani 120,000 nchi nzima,” amesema Mbussi.
Mkazi wa Mbeya akiwa na bidhaa za mkonge baada ya kununua katika Banda la Bodi ya Mkonge Tanzania lililoko kwenye Maonesho ya Nanenane viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya.
Ameitaja mikakati hiyo kuwa ni kugawa miche bure kwa wakulima katika wilaya mbalimbali nchini, kununua mitambo ya kuchakata mkonge wa wakulima, utafutaji masoko, kutoa elimu na kuhamasisha wakulima wengi kulima zao hilo.
Ofisa Kilimo katika bodi hiyo, Emmanuel Lutego, amesema zao hilo linahimili ukame na mkulima huanza kuvuna baada ya miaka mitatu hadi 18 ambapo kila mwaka huvuna mara mbili.
“Kutokana na mabadiliko ya tabianchi kilimo cha mkonge ni fursa kwa sababu zao hili linahimili ukame, ukipanda mche utaanza kuvuna baada ya miaka mitatu na kwa mwaka unavuna mara mbili kila baada ya miezi sita,” amesema Lutego.