UPATIKANAJI WA MAJI MJINI, VIJIJINI WAONGEZEKA
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira, Jackson Kiswaga, akizungumza wakati walipokutana na watendaji wa Wizara ya Maji kupata taarifa ya sekta ya maji na mwenendo wake hapa nchini.
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, amesema upatikanaji wa maji mjini na vijijini umeongezeka kwa kipindi cha Julai 2022 hadi Julai 2023.Kwa mjini umeongezeka kwa wastani wa asilimia 88 huku vijijini ukiongezeka kwa asilimia 77 na ukitarajiwa kufikia asilimia 80 Desemba 2023.
Akizungumza leo Agosti 15, 2023 wakati wa kikao cha pamoja na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira, amesema kwa mjini unatarajiwa kufika asilimia 91 Desemba 2023.
Kamati hiyo imekutana na Wizara ya Maji na kupata taarifa ya sekta ya maji na mwenendo wake hapa nchini.
Waziri Aweso amesema nia ni kufika lengo la asilimia 95 mjini na asilimia 85 vijijini, na sekta ya maji ipo tayari kwa maoni na ushauri wa Kamati ya Maji na Mazingira ili kufanikisha lengo hilo.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Jackson Kiswaga, ameipongeza sekta ya maji kwa kazi kubwa inayofanyika katika miradi ya maji ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma endelevu na kuleta mabadiliko katika jamii.


